Daktari Bingwa wa magonjwa ya wanawake, Dk. Wilbroad Ntuyabaliwe, amefariki dunia katika hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam.
Dk. Ntuyabaliwe, pichani, alifariki dunia Jumatatu iliyopita.
Wakati wa uhai wake, Dk. Ntuyabaliwe, aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali katika utumishi wake wa umma ikiwemo Ukurugenzi wa Huduma za Hospitali katika Wizara ya Afya kati ya mwaka 1978 hadi 1986, Mhadhiri Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hurbert Kairuki, jijini Dar es Salaam.
Pia, aliwahi kuwa Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili kati ya mwaka 1973 hadi 1977.
Kadhalika, marehemu aliwahi kufanya kazi katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kati ya Januari, 1977 na Februari, 1978.

Marehemu ambaye atakumbukwa kwa uadilifu na ushapa kazi bora pia aliwahi kuwa Mganga Mkuu Hospitali ya Tukuyu, mkoani Mbeya kati ya mwaka 1966 na Januari, 1969 na aliwahi kuwa Mrajisi wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya kuanzia Mei hadi Septemba 1966.
Dk. Ntuyabaliwe aliyezaliwa mwaka 1937 mkoani Kigoma, alipata shahada yake ya kwanza ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Makerere mwaka 1965 na shahada yake ya pili ya udaktari pia aliipata katika chuo hicho mwaka 1973.
Marehemu Dk. Ntuyabaliwe ameacha watoto watatu Shimmy, Jessy na Jacqueline.
CHANZO: NIPASHE