UMOJA wa Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi (MUWAZA) wenye makao makuu yake Denmark, umetoa vifaa mbalimbali kwa Hospitali ya Mnazi Mmoja vyenye thamani ya Sh milioni 80 kusaidia sekta ya afya.

Mwenyekiti wa umoja huo, Dk. Omar Juma Khatib alikabidhi vifaa hivyo kwa ajili ya matumizi ya wadi ya wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu (ICU).

Dk. Khatib alisema wameamua kutoa msaada huo kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya afya kwa wananchi wa Zanzibar ikiwemo ICU ambayo ipo katika hali mbaya kutokana na uchakavu wa vifaa vyake.

“Msaada huu ni kutoka kwa Wazanzibari waliopo nje ya nchi kwa ajili ya ndugu zao wa Zanzibar....baadhi ya vifaa tulivyoleta ni kwa ajili ya wadi ya wagonjwa mahututi,” alisema Dk. Khatib.

Mapema akipokea msaada huo, Katibu wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Hassan Hafidh alisema msaada huo umekuja katika wakati muafaka kwani hospitali hiyo inakabiliwa na ukosefu wa vifaa mbalimbali.

“Tunawashukuru kwa dhati umoja wa Wazanzibari waliopo nje ya nchi kwa msaada wao ambao umekuja katika wakati muafaka huku hospitali ikikabiliwa na ukosefu wa vifaa mbalimbali,” alisema Hafidh.

Wadi hiyo ya wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu kwa sasa ipo katika matengenezo chini ya Wizara ya Afya ambapo hivi karibuni vifaa mbalimbali ikiwemo vitanda vinatazamiwa kuwekwa.