Wakati wagombea wa vyama vinane vikirejesha fomu hizo, mbombea wa Union For Multiparty Democracy (UMD), alishindwa kuirejesha fomu yake kwa Msimamizi wa Uchaguzi huo, Protace Magayane.
CUF, CHADEMA WAFANYIANA VURUGU
Wagombea wa Chadema na CUF, walirejesha fomu hizo jana kati ya saa 7:00 mchana na saa 9:00 mchana kwa maandamano makubwa yaliyoanzia katika ofisi za vyama vyao zilizopo katikati ya mji wa Igunga.
Hata hivyo, iliibuka tafrani baada ya wafuasi wa vyama hivyo kutaka kushambuliana kila upande uliulalamikia mwingine kwamba ulitaka kuvuruga msafara wake.
Kabla ya maandamano ya Chadema kuanza msafara wa CUF ambao ulikuwa katika magari ulisimama kwa muda kando ya barabara kuu iendayo Nzega.
Wakati CUF wakiwa wamesimama kandokando ya barabara hiyo, wafuasi wa Chadema waliokuwa katika ofisi za Makao Makuu ya Wilaya ya Igunga, walikuwa wakijiandaa kuanza maandamano.
Kwa zaidi ya nusu saa, CUF walikuwa bado wamesimama kando kando ya barabara hiyo, hali ambayo ilizua tafrani na wafuasi wa vyama hivyo kurushiana maneno.
OCD AWAITA VIONGOZI
Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Igunga (OCD), Issa Isimail, jana jioni aliwaita viongozi wa Chadema na CUF ofisini kwake kujadiliana kuhusu vurugu zilizotaka kuibuka wakati wa kurejesha fomu za wagombea wao.
Katika kikao hicho CUF kiliwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu, Bara, Julius Mtatiro, wakati Chadema kiliwakilishwa na Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo, Benson Kigaila.
KAULI ZA KASHINDI WA CHADEMA
Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu, Mgombea wa Chadema, Joseph Kashindi, aliahidi kufanya kampeni za kistaarabu na kwamba shamrashamra hizo zinaonyesha kukubalika kwake na kwa chama chake.
“Mimi naona kuwa chama hicho (CUF), kimefanya kitu ambacho si ustaarabu, kwa sababu wametukatisha mara mbili ingekuwa mara moja tungesema labda ni coincidence (bahati mbaya tu), lakini wamekwenda wakazunguka mara ya pili tena, wakakatiza msafara wetu na bado wametukuta katika ofisi ya msimamizi wamevamia mle tukiwa bado tunahudumiwa, hawajaonyesha ustaarabu,” alisema.
Alipoulizwa kwa hali kama hiyo wananchi watakuwa na imani na vyama vyao, alisema: “Wananchi wa Igunga ni watu waliokomaa kisiasa, lakini pia kifikra wataona chama gani kina matatizo, sisi kama Chadema hatuna tatizo na tunaomba wananchi wetu wasianzishe aina yoyote ya vurugu, waache watu wengine wafanye hizo vurugu.”
Kuhusu tatizo la daraja la Mbutu ambalo limeshaahidiwa kutengenezwa na mbunge aliyepita kwa zaidi ya miaka mitano, aliwaomba wananchi wa Igunga, waamini kuwa wamepata mtetezi wa kweli ambaye ana uchungu na matatizo yao.
“Nikijua kuwa sehemu ya Kaskazini ya Igunga ina uchumi mkubwa ambao husababisha mzunguko mkubwa wa pesa katika mji wetu, nitapigania kwa hali na mali kuhakikisha kuwa daraja hilo linajengwa,” alisema.
Akizungumzia sakata hilo, Ofisa Uchaguzi wa CUF, Maole Kuchilingulo, alikanusha kuingilia msafara wa Chadema na kwamba wao walikuwa na safari yao ambayo ilikuwa ikiwalazimu kuvuka barabara kuu iendayo Nzega na kuzunguka kurudi tena mjini.
“Lengo lilikuwa ni kuwatangazia wananchi kwamba tunarudisha fomu za mgombea wetu…sasa kuna watu walisimama barabarani kutublock (kutuzuia)…basi sisi tukaforce (tukalazimisha) njia tukapita kwa sababu its was our right (haki yetu) na tulikuwa tunakwenda na muda kuhakikisha saa 10:00 tunarudisha fomu zetu,” alisema.
Maole alisema zoezi la kurejesha fomu limeleta uchangamfu katika mji wa Igunga na limeonyesha kuwa kuna siasa mpya,” alisema.
KAULI ZA MAHONA WA CUF
Mgombea wa CUF, Leopard Mahona, alisema kipaumbele kikubwa kwake endapo atachaguliwa, kitakuwa ni kushughulikia tatizo la maji ambalo limekuwa likiwatatiza wananchi wa Igunga kwa muda mrefu.
Aliongeza kipaumbele kingine kitakuwa ni kushughulikia matatizo yanayozikabili sekta za mifugo, kilimo pamoja na matatizo mengine.
Kuhusu mvutano na wafuasi wa Chadema, alisema: “Halinipi shida, hizo nyingine zote ni mbwembwe ila wananchi wa Igunga wanamjua mbunge wao kwa sababu mwaka huu nadhani wananchi wa Igunga wanachagua mwanachi mwenzao na mwananchi mwenzao anatoka kwenye chama chao chama cha wana-Igunga ni Chama cha Wananchi (CUF),” alisema.
Mwenyekiti wa Vijana wa CUF Taifa, Mohamed Babu, alisema wakati wanajiandaa na zoezi la kurejesha fomu Chadema waliwaingiza wanachama wao barabarani ili wasiweze kupita.
“Laiti kama sisi tungekosa busara amani pale ingevurugika, tunachukua nafasi hii kutoa wito jamani tufanye uchaguzi wa demokrasia na amani hatuna sababu ya kuanza kugombana…Tunawaomba Chadema wafanye siasa za kistaarabu wakati wa vurugu umekwisha, ”alisema.
KAULI ZA DK. KAFUMU WA CCM
Kwa upande wake mgombea wa CCM, Dk. Peter Kafumu, alisema anategemea ushindi mkubwa.
“Mimi kwa maoni yangu na kwa matumaini yangu nategenea ushindi kwa sababu nimekuja kugombea kwenye kura za maoni zaidi ya mara tatu na wananchi wananifahamu na najua wale waliokuwa upande mwingine watakuwa upande wangu,” alisema.
“Kwa maana hiyo nafahamika na najua nitapata ushindi wa kishindo hali inaonyesha hivyo kwa sababu kila ninakokwenda nafahamika na wananchi wananipokea vizuri,” aliongeza.
Aliwataka wananchi wa Igunga kutokuwa na hofu ya kumchagua kwa kuwa atakuwa mgombea anayestahili kuchaguliwa kofauti na wenzake kutokana na kuwa na uzoefu katika mambo mbalimbali.
“Mimi napenda kuwaeleza kuwa wasiwe na wasiwasi wa kunichagua, watakuwa wamepata mbunge anayestahili kwa maana ya uzoefu katika serikali, medani za kimataifa, usomi pia nimesoma vizuri nayafahamu mambo ya kimataifa na pia ni mtoto wa huku,” alisema na kuongeza:
“Nayafahamu matatizo yao nimeishi huku nimechunga ng’ombe najua nitaweza kushirikiana nao kuyatatua matatizo yote yale yaliyoko katika wilaya yetu hasa yale yaliyobakia baada ya mengine mengi kuwa yamefanywa na mbunge aliyepita.”
Alisema kipaumbele chake kitakuwa ni kutatua matatizo ya maji kwa kuongeza mabwawa, kutengeneza barabara na hasa za vijijini ambazo zimekuwa hazipitiki, ujenzi wa daraja la Mbutu pamoja na kuboresha sekta ya elimu.
Mratibu wa kampeni za CCM, Mwigulu Nchemba, alisema CCM imeheshimu mawazo ya wanachama wake kwa kukubaliana na kura za maoni walizopiga.
“Tunawaelezea ukweli wenzetu wa uhalisia wa mambo, huo ndio ukweli kwamba duniani kote baada ya uchaguzi kufanyika na serikali imeshatengenezwa vyama vyote huwa vinatekeleza sera ya chama chenye serikali,” alisema.
“Niwashukuru sana wana-Igunga kwa kutuunga mkono kwa kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kilichopita na kwa kuridhia leo (jana), kwamba kwa kuwa bado tuna siku chache baada ya msiba turudishe fomu kwa hali ya utulivu tu kama hivi. Niombe wajitokeze kwa wingi siku ya uzinduzi, siku ya uzinduzi tu itatoa picha,” alisema.
Mbali na CCM, CUF na Chadema, wagombea wa vyama vingine waliorejesha fomu zao jana ni wanane wa Chausta (Hassan Ramadhan) ambaye alikuwa wa kwanza jana na kufuatiwa na na mgombea wa UPDP, Hemed Ramadhan.
Wengine ni Said Makeni (DP), John Maguma (SAU) na Stephen Mshuli (AFP).
NDIGAYANE WA UMD AKWAMA KUREJESHA FOMU
Wakati wagombea wanane wakirejesha fomu zao na kupokewa na Mgayane, mgombea wa UMD, Lazaro Ndigayane, alishindwa kurejesha fomu yake.
Akizungumza na waandishi wa habari, Ndigaye alisema ameshindwa kurejesha fomu kutokana na kukosa ushirikiano kutoka makao makuu ya chama chake.
Aliitaja sababu nyingine kuwa ni kukosa fedha kwa ajili ya kufanya kampeni.
Magayane alisema mwisho wa kurejesha fomu ulikuwa jana saa 10:00 jioni ambapo fomu hizo zitabandikwa ubaoni kwa ajili ya watu walio na pingamizi kuwasilisha.
“Tunatoa saa 24 kwa ajili ya watu walio na mapingamizi waweze kuyawasilisha,” alisema Magayane.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Oktoba 2, mwaka huu kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Rostam Aziz, aliyejiuzulu Julai 13, mwaka huu kwa maelezo kuwa amechoshwa na siasa uchwara, fitina na kuandamwa ndani ya CCM. Rostam pia alijiuzulu nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia Mkoa wa Tabora.
CHANZO: NIPASHE
0 Comments