Mkuu wa wilaya ya Igunga Mh; Fatuma Kimario.
WANAZUONI wa Kiislamu nchini wameipa siku tatu Chadema Taifa kulaani kitendo cha wafuasi na viongozi wake kulidhalilisha vazi tukufu la hijab na kumwomba radhi Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario, kwa kumvua sitara yake.
Wamesema iwapo chama hicho kitapuuza kufanya hivyo na kupita muda huo wanazuoni hao na Waislamu wataiona Chadema kama chama chenye sera na madhumuni ya kuhujumu Uislamu na Waislamu wa Tanzania na kuhimiza Waislamu kukiepuka kama ukoma.
Kauli hiyo iko kwenye tamko la Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania (HAY-AT) lililosomwa jana na Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti Kuu ya Umoja huo, Shehe Sherali Hussein Sherali na kusema siku tatu hizo zilianza jana.
Wanazuoni hao zaidi ya 10 wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Shehe Suleimani Kilemile, walitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari na kusema baada ya hapo umoja huo utakaa na kutafakari hatua stahiki za kukabiliana na dharau hizo na kuelekeza Waislamu cha kufanya.
Sherali alisema ifahamike, kwamba shambulio lolote dhidi ya hijab ni dhidi ya Uislamu na Waislamu wote, haliwezi kuvumilika na watakabiliana na yeyote anayetaka kuidhalilisha amri ya hijab iliyo katika Quran sura ya 33:59.
“Tunataka ifahamike, kwamba yeyote atakayelidharau vazi la hijab kwa kauli au vitendo, atakuwa amewachokoza Waislamu na sisi kamwe hatukubali hilo liendelee na kukaa kimya, tutachukua hatua stahiki na ikibidi tutalazimika kuondoa munkari kwa mikono yetu wenyewe, kama dini yetu inavyotuelekeza,” alisema.
Aliongeza kuwa wanalaani na kupinga kitendo kilichofanywa na wanaodaiwa kuwa wafuasi na viongozi wa Chadema kumvua nguo Mkuu huyo wa Wilaya na kumwacha bila sitara.
Alisema Kimario ni Mwislamu anayefuata mafundisho ya Uislamu yanayomtaka kila
mwanamke ajisitiri kwa vazi la hijab, hivyo kumvua ni kumdhalilisha kwa wanajamii kama mwanamke wa Kiislamu, mama mwenye watoto na kiongozi wa Serikali.
Tumetafakari tukio hili kwa undani na tunalichukulia kama shambulio la wazi na la makusudi dhidi ya mafundisho yetu na dini ya Kiislamu, yanayomtaka kila mwanamke aliyevunja ungo, kujisitiri kwa kuvaa vazi la hijab,” alisema Sherali.
Aliwaomba Watanzania wote, wanaharakati wa asasi za kijamii na wa haki za binadamu, viongozi wa vyama vya siasa na wa dini zote, kulaani na kupinga unyanyasaji huo wa kijinsia na kidini unaokwenda kinyume na Katiba ya nchi na utamaduni wa Watanzania wa kuheshimiana.
“Tumesikitishwa na ukimya wa asasi za kijamii zinazodai kutetea haki za binadamu na za wanawake, kutolaani kitendo hiki cha mwenzao kudhalilishwa kijinsia, kuendelea kukaa kimya kunatulazimisha kuwaona wanafiki na ndumilakuwili juu ya madai yao ya kutetea wanawake,” alisisitiza.
Alisema wanaitaka Serikali ilitafakari kwa kina tukio hili la kudhalilishwa mwanamke Mwislamu, akilitumikia Taifa kama mmoja wa viongozi wake, kukaa kimya kutatoa tafsiri hasi juu ya jinsi inavyolichukulia tukio hilo na kuitaka kuwachukulia hatua kali wahusika.
Wanawake Waislamu Katika hatua nyingine, kikao cha wanawake Waislamu kilichofanyika kwenye ukumbi wa Karimjee Jumapili, wanawake walilaani tukio hilo.
Kikao hicho chini ya Mwenyekiti wake Fatma Juma, kiliwataka wanawake na wapenda amani wote kulaani kitendo hicho cha udhalilishaji wanawake.
Walisema kitendo hicho kimeonesha dharau, si tu kwa Uislamu, bali hata kwa madhehebu mengine na kinaweza kuvuruga amani na utulivu uliopo nchini hivi sasa.
Tamko la kikao hicho, lilisema litaanza kusambazwa katika misikiti yote Ijumaa, ili Waislamu waelewe namna walivyoguswa na kusononeshwa na tukio hilo.
Shura ya Maimamu
Habari zaidi zilizopatikana zilisema Shura ya Maimamu nayo itakutana hivi karibuni kujadili tukio hilo la mwanamke wa Kiislamu kuvuliwa hijab.
Mbali ya kukutana huko, Shura hiyo itaandaa maandamano ya kupinga kitendo hicho ambacho wamekitafsiri kuwa ni matusi dhidi ya Uislamu.
Katibu wa Shura ya Maimam, Shehe Ponda Issa Ponda, jana alithibitisha kuwapo kwa ajenda hiyo.
Akizungumza na gazeti hili jana alisema kitendo kilichofanywa na wafuasi wa Chadema kimekosa utu, ustaarabu, uungwana na maadili mema na kinapaswa kukemewa na wapenda amani wote nchini, bila kujali itikadi zao, kwani kikiachwa kitazidi kukomaa na kuonekana ni
jambo la kawaida katika jamii.
Akizungumzia kadhia hiyo, Katibu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini (Baraza Kuu), Shehe Ramadhan Sanze, naye alisema taasisi yake inaungana na wanaolaani tukio hilo .
“Mtazame DC Fatuma namna alivyokuwa akivutwa, akivuliwa nguo na akitukanwa na vijana wale wa Chadema ambao baadhi yao ni sawa na watoto wake wa kuzaa, hakika inatia uchungu,” alisema Shehe Sanze kwa masikitiko na kuongeza kuwa wanawake kote nchini wamedhalilishwa kwa uhuni ule.
Nao baadhi ya Waislamu ndani ya Chadema wameeleza kukasirishwa na kitendo hicho cha wenzao kumvua kwa nguvu hijab Mkuu wa Wilaya.
Waislamu hao ambao hawakutaka kutajwa majina, walisema watakutana hivi karibuni kujadiliana juu ya hatua za kuchukua kutokana na tukio hilo la kudhalilisha dini yao.
Kwa karibu wiki nzima baada ya tukio hilo la Igunga watu mbalimbali wametuma salamu zao za kulaani tukio hilo kupitia Radio Imani ya Morogoro na Radio Kheri na Radio Quran.
Viongozi watatu wa Chadema wakiwamo wabunge wawili wamefikishwa mahakamani Tabora, wakikabiliwa na mashitaka manne ya wizi wa simu, shambulio, matusi ya nguoni na utekaji
nyara. Kesi yao iliahirishwa juzi hadi Oktoba 10.
Chadema wang’aka
Akizungumzia tuhuma hizo jana, Mwanasheria wa Chama cha Chadema Tundu Lissu alisema hawajapata taarifa ya suala hilo na kuwataka wanazuoni hao kufahamu kuwa Mkuu wa Wilaya hakuvuliwa hijab na wala hakudhalilishwa kama inavyodaiwa.
Alisema ushahidi wa suala hilo unaonekana katika kesi waliyofunguliwa wanachama hao na hakuna tuhuma za kumdhalilisha kijinsia wala shambulio la aibu.
“Hatuna chochote cha kuomba msamaha kutokana na hali halisi ilivyokuwa, labda kama ingekuwa kweli alivaa hijab,” alisema Lissu.
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa picha, Mkuu huyo wa Wilaya alikuwa amevaa mtandio, gauni linaloishia magotini na lenye mikono mifupi wakati hijab anavyoelewa yeye ni nguo inayofunika mwili mzima isipokuwa uso.
0 Comments