Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, jana alizindua kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Igunga, mkoani Tabora, huku akimshambulia Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.
Profesa Lipumba katika mashambulizi yake dhidi ya Mkapa, alimshutumu kuwa aliiuza nchi kwa bei poa kutokana na mikataba mibovu ambayo serikali iliingia wakati wa utawala wake.
Aidha, alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama kingekuwa ni chama makini kisingekubali aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, ajiuzulu na kufanyika kwa uchaguzi mdogo.
Rostam alijiuzulu ubunge na ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Julai, 13 mwaka huu kwa maelezo kuwa amechoshwa na siasa uchwara, fitina na kuandamwa ndani ya CCM.
Profesa Lipumba, aliyasema hayo wakati akimnadi mgombea wa chama chake katika uchaguzi huo, Leopard Mahona, katika uzinduzi rasmi wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Sokoine mjini Igunga.


Profesa Lipumba, alisema Tanzania ni nchi ya tatu kwa kuuza dhahabu nje kwa wingi, lakini fedha zote ya madini hayo zinachukuliwa na makampuni ya nje.
“Fedha yote kwa sababu ya mikataba mibovu wanataka hata maeneo mengine ya Igunga yenye dhahabu yauzwe kwa makampuni ya nje,” alisema na kuongeza:
“Na Mkapa ndiye alianzisha utaratibu wa kuuza nchi yeye wakati wake ndipo ilisainiwa mikataba ambayo hata Benki ya Dunia, hata Shirika la Fedha la Kimataifa kwenye ripoti ya uchumi kuhusu Tanzania wanamlalamikia”.
Wanasema inakuaje serikali ya Tanzania haipati kodi yoyote kutoka kwenye madini,” alisema Profesa Lipumba katika mkutano huo.
Alisema kwa mwaka dhahabu inayouzwa nchi za nje ni zaidi ya Dola za Marekani bilioni 1.5 na kuongeza kuwa alisema kwenye mauzo ya Sh. 100, serikali inaambulia Sh. tatu.
“Mkapa ndiye kaiuza nchi hii na ufisadi mkubwa mkubwa umeanza wakati wa utawala wa Mkapa, ufisadi wa rada kununua rada bomu Dola milioni 40 wakati rada inayokidhi mahitaji ni Dola milioni tano za Kimarekani, ulifanyika wakati wa Mkapa, mikatapa ya IPTL (Kampuni ya Kufua Umeme) inatuuzia umeme gharama kubwa,” alisema.
Profesa Lipumba aliwaambia wananchi kuwa Mkapa alishauriwa avunje mkataba huo akakataa na kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati huo alikuwa ni Andrew Chenge, na kuongeza kuwa hata ununuzi wa ndege ya rais ulifanyika wakati Mkapa akiwa rais.
Pia, alisema kuwa mabilioni ya fedha za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje Nje (EPA) yalichotwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wakati wa uongozi wa Mkapa.
AMZUMGUMZIA ROSTAM AZIZ
Akizungumzia kuhusiana kujiuzulu kwa Rostam Aziz, Profesa Lipumba alisema ingawa uchaguzi mdogo una gharama kubwa, lakini CCM kimeruhusu mbunge huyo kujivua gamba na kuitishwa kwa uchaguzi mdogo.
Hata hivyo, alisema kuwa serikali ya CCM imekuwa ikitangaza kuwa kuna matatizo ya fedha, bajeti tegemezi, huduma nyeti hazipatikani na miundombinu ni mibovu.
“Kama chama tawala kingekuwa chama makini na jimbo la Igunga lipo chini ya chama tawala, chama makini kisingeruhusu kupoteza mbunge wa Igunga pawepo na uchaguzi mdogo ni kwa sababu CCM haina dira na inaendesha siasa za kupakana matope kama Rostam alivyosema wakati akijiuzulu ubunge,” alisema.
Profesa Lipumba aliwaomba wananchi wa Igunga, kumchagua Mahona ili aende bungeni kupambana na ufisadi na mikataba mibovu inayosainiwa na serikali ya CCM.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Bara, Julius Mtatiro, aliwataka wananchi hao kupiga kura za ndio kwa Mahona ili akawawakilishe na kuwatetea bungeni.
“CCM wanawadanganya watu wakamchague mgombea maarufu, Wanaigunga mnahitaji mtu wa kuwatatulia matatizo yenu na huyo si mwingine ni Mahona ana umri wa miaka 29, hao wengine wanataka kwenda bungeni kutafuta pensheni,” alidai.
MAHONA AOMBA KURA ATATUE MATATIZO
Naye Mahona aliwaomba wananchi wampe ridhaa ya kuwaongoza katika jimbo hilo ili aweze kushirikiana nao katika kutatua matatizo.

MAANDAMANO YAIPAMBA IGUNGA
Mkutano huo ulitanguliwa na maandamano yaliyoanzia kilometa tatu kutoka katika mji wa Igunga ambayo yalimshirikisha Profesa Lipumba na viongozi wengine wa chama hicho.
Maandamano hayo yalipambwa na mabango mbalimbali ambayo baadhi yake yalibeba ujumbe kuwa Mahona Sauti ya Wananchi, Mahona wa hapahapa, Tunasema na kutenda, CUF kiboko cha mafisadi na Igunga ni mali ya CUF.
Pia Profesa Lipumba , Mahona na viongozi wengine wa juu wa chama hicho walipanda katika mkokoteni wa kukotwa na Punda wawili.
Kabla ya kuanza kwa mkutano huo, vikundi mbalimbali vya kwaya kutoka katika kata mbalimbali za Igunga na msanii wa mashairi Mzee Rashid Sultan Manjunju alikosha nyoyo za wasikilizaji.
Mgombea huyo pia alikabidhiwa Mkuki, upinde na mshale, kuvishwa mgolole na kisha kukalishwa katika kigoda kabla ya kupakwa unga wa mtama usoni kama ishara ya kumtakia mema katika safari yake ya kuusaka ubunge.
CHANZO: NIPASHE