MWANDISHI WETU, Nairobi
IDADI ya waliofariki nchini Kenya kutokana na moto mkubwa uliozuka juzi jijini Nairobi baada ya bomba la mafuta kulipuka, sasa wamefikia 120.
Hofu imetanda nchini humo kwamba huenda idadi ya watu waliofariki juzi ikaongezeka zaidi kutokana na hali za wagonjwa hao kuwa mbaya huku wengine zaidi ya 160 wakihitaji matibabu ya haraka, kutokana na kuungua vibaya.
Mratibu wa Shirika la Msalaba mwekundu, Pamela Indiaka alisema inawezekana idadi ya watu waliofariki ikaongezeka baada ya kuokota miili ya wengine hapo jana.Maafa hayo yalitokea katika mtaa wa mabanda wa Sinai uliopo karibu na sehemu ya Viwanda ya Lunga Lunga, jijini Nairobi.
Msemaji wa polisi nchini humo, Thomas Atuti jana alisema idadi ya waliofariki kutokana na moto huo ni zaidi ya watu 120.
Atuti alisema chanzo cha moto huo ni sigara iliyowashwa na mmoja wa watu waliojitokeza kuiba mafuta kutoka kwenye bomba la mafuta lililokuwa likikatiza kitongoji cha Sinai kuelekea Uwanja wa Ndege.
Kwa mujibu wa msemaji huyo wa polisi, bomba hilo lilikuwa likivuja mafuta hali iliyowafanya baadhi ya watu wamiminike na ndoo zao kuja kukinga mafuta.
Mlipuko mkubwa ulioambatana na moto mkubwa uliosambaa kwenye kitongoji hicho na kusababisha watu wengi kuungua na moto.Alisema katika tukio hilo watoto wengi ndio waliofariki kwenye moto huo.
Baadhi watu walijitosa kwenye mto ili kunusuru maisha yao lakini wengi wao walisombwa na maji.
Juzi jioni, Waziri Mkuu, Raila Odinga alitembelea eneo hilo ambako hata hivyo, alikutana na vurugu kubwa baada ya wananchi wakiwamo waliofiwa na ndugu zao kutaka kuvamia eneo hilo lenye bomba la mafuta wakituhumu kwamba ndiyo chanzo.
Tukio baya kama hilo liliwahi kuikumba Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), ambako mwaka jana watu 230 walifariki kutokana na mlipuko katika bomba la mafuta.
0 Comments