Eneo takatifu la waumini wa madhehebu ya kishia nchini Iraq.

Mahujaji 22 wa madhehebu ya kishia wameuawa katika mkoa wa Anbar, magharibi mwa Iraq, maafisa wa Iraq wanasema.
Inasemekana kuwa wanaume hao walikuwa wakisafiri kwa basi kuzuru mahali patakatifu nchini Syria waliposimamishwa katika kizuizi kimoja kilichoko jangwani.
Maafisa wanasema wanawake waliamriwa kutoka nje ya basi na wanaume wakapelekwa hadi sehemu nyingine na kuuawa.

Wanaume walichukuliwa na wanawake kuachwa

Mashambulio dhidi ya mahujaji wa kishia yamesababisha mauaji ya mamia ya watu katika miezi ya hivi karibuni.
" Kulikuwa na basi kubwa na basi dogo na watu 30, ikiwemo wanaume 22 na wanawake 8," Meja Jenerali Hadi Razij, mkuu wa polisi mkoani humo, aliambia shirika la habari la Reuters.

" Walichukua wanaume na wakawaacha wanawake."

Waliouawa walikuwa wenyeji wa Karbala

Tukio hilo lilifanyika kusini mwa mji wa Rutbah, chanzo kimoja cha usalama kilichonukuliwa na Reuters kilisema.
Shirika la habari la Associated Press linasema wanajeshi wa Iraq waliokuwa wanashika doria waliwakuta wanawake wakiwa kando ya barabara.
Wote waliouawa wanasemekana kuwa wenyeji wa mji wa Karbala.