Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kueleza alivyoshambuliwa na kudhalilishwa na viongozi na wafuasi wa Chadema katika eneo la Isakamaliwa.(Na Mpigapicha Wetu).

MKUU wa Wilaya ya Igunga, Fatma Kimario amesimulia jinsi alivyovuliwa nguo, kupigwa na kudhalilishwa kijinsia na vijana pamoja na viongozi wa Chadema na kusema kuwa binafsi ameachwa uchi na familia yake imeathirika kisaikolojia.

Kutokana na udhalilishaji huo, ambao umeonekana hata katika picha za magazeti mbalimbali, Polisi wilayani Igunga imewakamata Mbunge wa Maswa Mashariki, Kasulumba Sylvester na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Morogoro, Suzan Kiwanga.

Akisimulia hali iliyomtokea huku akionesha picha za magazeti za tukio hilo, Kimario alisema kwa utamaduni wake, hata siku moja hawezi kuacha hijab au mtandio mbele ya watu, lakini alivuliwa na kupandishwa nguo zake juu na kuachwa sehemu za mwili wake wazi.

"Waliingia ndani ya ofisi (ya Mtendaji wa Kijiji cha Isakamaliwa), yule Mbunge Sylvester akasema DC yuko wapi?

Mtendaji akajibu hayupo, lakini kijana mwingine akasema huyo hapo.

"Nilikuwa nimekaa kwenye kiti, Sylvester akasema malaya mkubwa we, ndiye niliyetaka kuzaa na wewe...akanivuta mkono wa kulia na kijana mwingine akanishika mkono wa kushoto wakanivuta nje ya ofisi," alisimulia Mkuu huyo wa Wilaya.

Katika purukushani hiyo, alisema kijana mmoja alikuwa akimpiga kichwani, akamvua mtandio na hijab na Mbunge huyo wa Maswa alimvuta blauzi na kuacha sehemu kubwa ya tumbo lake nje, jambo alilolifananisha na jaribio la ubakaji.

"Hii ni sawa na ubakaji, kumpandisha mtu nguo, kwangu mimi wamenivua nguo na kuniacha uchi," alisema mkuu huyo wa wilaya.

Mama huyo wa makamo, alisema kutokana na hali hiyo, yeye na familia yake wameathirika kisaikolojia na pia alilazimika kwenda hospitali kutokana na kupata maumivu sehemu za kichwani na mikononi.



Alipoulizwa kwa nini hakusindikizwa na polisi, alisema alipaswa kuwa na polisi wawili, lakini imekuwa bahati hawakuwepo kwa kuwa wangefyatua risasi na kusababisha mauaji ingawa
wasingeweza kuzuia.

Alisema hata sungusungu walikimbia kwa kuwa umati ulikuwa mkubwa. Baada ya kutolewa nje kwa mujibu wa madai yake, walitaka kumbeba juu juu kumpeleka kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa ili akamsalimie, lakini alikataa kwa maelezo kuwa Dk. Slaa ndiye aliyepaswa kwenda kusaini kitabu cha wageni alipoingia Igunga, jambo ambalo hakufanya.

"Niliwaomba, nikawaambia mkinibeba mtaniacha uchi, wakaniweka chini ya mti huku nikilindwa na vijana na Suzan mpaka Dk. Slaa alipomaliza mkutano wakaniachia," alidai.

Katika mkutano huo, DC alidai Dk. Slaa alitangaza kumfukuza kazi yeye kwa madai ya kumkuta akipiga kampeni, wakati alikuwa katika shughuli zake za kikazi na wakati huo saa nane mchana, Chadema hawakuwepo katika eneo hilo na ratiba ya kampeni ilikuwa ikionesha Chadema walipaswa kuwa wamemaliza mkutano wao uliotakiwa kuanza saa 4 asubuhi mpaka saa 6.

Tundu Lissu aenda kuwatetea Wakati Kimario akielezea hali ilivyokuwa na athari zake kwake na katika familia yake, taarifa zilisambaa kuhusu kushikiliwa kwa wabunge hao wa Chadema.

Gazeti hili lilifika katika Kituo cha Polisi Igunga na kukuta askari wa kutuliza ghasia wakiwa wamekizunguka wakiwa na silaha pamoja na gari la maji ya kuwasha pamoja na baadhi ya viongozi wa Chadema, akiwemo mmoja wa waratibu wa kampeni za chama hicho, Waitara Mwita.

Baada ya muda, Mwanasheria wa Chadema na Mbunge wa Iramba Mashariki, Tundu Lissu alitoka katika kituo hicho na kudai chama hicho kinafanyiwa njama ya kupunguza kasi ya kampeni zake ndio maana Kasulumba aliyedai ndiye meneja wa kampeni, kakamatwa.

Lissu alidai amemsikia Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathimini wa Polisi, Makao Makuu ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Isaya Mngulu, akisema hawatawaachia wabunge hao mpaka watakapotaja majina ya wenzao walioshirikiana katika udhalilishaji huo.

Alidai ni njama kwa madai kuwa hata Polisi hawakwenda kulinda mkutano wao wa hadhara, ingawa Mngulu katika maelezo ya juzi, alisema ratiba ya kampeni ilionesha kuwa Chadema walipaswa kufanya kampeni saa 4 hadi saa 6 na polisi walikwenda lakini hawakuona hata dalili za mkutano huo.

Chadema badala yake walikwenda saa 8 mchana. Kamanda Mngulu alipotafutwa kwa simu, alikiri kuwakamata wabunge hao wawili na raia mmoja, Anwari Kaswega na kuongeza kuwa watafikishwa mahakamani Jumatatu.