Kikosi cha Yanga ya Dar es Salaam.
BAADA ya kupata ushindi wake wa kwanza wa Ligi Kuu dhidi ya African Lyon katikati ya wiki, Yanga leo Jumapili inashuka uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuwavaa Azam FC, huku vinara wa ligi hiyo Simba wakiwa ugenini kucheza na Kagera Sugar.

Yanga imeongezewa nguvu kwa ujio wa mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Kiiza, aliyewasili nchini juzi tayari kwa kuivaa Azam FC.

Kiiza alikuwa akiwaumiza vichwa viongozi na mashabiki wa Yanga, kwani aliondoka nchini wiki mbili zilizopita kwa ajili ya kuitumikia timu yake ya taifa ‘The Cranes’ kwenye michezo ya All Africa Games iliyomalizika hivi karibuni nchini Msumbiji. 


<><> <><> <><> <><><><> <><> <><> <><>
Kikosi cha Azam Fc.
Mshambuliaji huyo alipaswa kuripoti katika timu yake ya Yanga tangu Alhamisi, lakini aliamua kubaki jijini Kampala, Uganda, huku akiwa hana mawasiliano na viongozi wake hali iliyoanza kuwaweka katika hali ya wasiwasi kwamba huenda asirudi tena.

Pia Yanga itakuwa na wakati mzuri zaidi, kwani beki wake mahiri, Nadir Harub ‘Cannavaro’, ambaye amekuwa nje ya dimba kwa mwezi mmoja baada ya kuumia wakati akiitumikia timu yake ilipocheza na mahasimu wao Simba kuwania Ngao ya Jamii, yuko fiti na anatarajiwa kuwepo kwenye mchezo huo.



Lakini mchezo huo hautakuwa rahisi kwa Yanga, kwani Azam inao wachezaji wazoefu ambao wanaielewa vizuri Yanga.

Mrisho Ngassa aliyepata kuchezea Yanga, John Bocco na viungo Ramadhan Chombo na Jabir Azi ni hazina ambayo Azam inaitegemea leo kuiua Yanga, pamoja na mshambuliaji raia wa Ivory Coast, Kipre Tchetche.

Azam inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi nane, huku Yanga ikiwa nafasi ya saba baada ya kujikusanyia pointi sita.

Simba inayoongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 13 itakuwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, kuivaa Kagera Sugar inayoshika nafasi ya kumi ikiwa na pointi nne, baada ya kutoka sare mechi nne.

Kagera Sugar haijashinda mechi tangu ligi hiyo ianze msimu huu ikiwa imefungwa mechi moja na kutoka sare nne. Ligi ina timu 14.

Hivyo leo timu hiyo ikiwa na mshambuliaji wake mahiri raia wa Uganda, Mike Katende itakuwa inahaha kujaribu kusaka ushindi.

Wakati huohuo, Waandishi Wetu wanaripoti kuwa timu za Coastal Union na Villa Squad zilizorejea Ligi Kuu msimu huu, mambo yameendelea kuwa magumu baada ya kupoteza mechi zao.

Coastal ilijikuta ikilala mabao 2-1 na Ruvu Shooting Uwanja wa Mlandizi mkoani Pwani, huku V illa ikifungwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.

Katika mchezo wa Coastal Union, mabao ya washindi yalifungwa dakika ya 16 na Ayoub Kitala na Seif Abdallah dakika ya 19, wakati la Coastal lilifungwa dakika ya 38 na Salum Gilla.

Kutokana na matokeo hayo, Ruvu Shooting imechupa kutoka nafasi ya 11 hadi ya sita ikiwa imefikisha pointi saba, wakati Coastal inashika nafasi ya 12 kati ya timu 14 zinazoshiriki ikiwa na pointi zake nne.

Katika mchezo wa Mtibwa na Villa, mabao ya washindi yalifungwa na Thomas Maurice dakika ya 13 na Said Rashid dakika ya 49.

Mtibwa Sugar iliyokuwa ikishika nafasi ya tatu imechupa hadi nafasi ya pili baada ya kufikisha pointi 11 na kuiacha JKT Ruvu ikiwa na pointi kumi baada ya jana timu hiyo kutoka 0-0 na Toto African Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.


<><> <><><><> <><> <><> <><>