MATUKIO ya moto jijini Mbeya yameendelea kutishia amani baada ya sehemu ya nyumba ya askari polisi iliyopo jirani na Kituo cha Kati jijini kuteketea.

Awali, zilienea taarifa jijini hapa kwamba kituo hicho cha polisi ndicho kimeungua moto hali iliyosababisha taharuki kwa wakazi na hivyo umati wa watu kukusanyika kushuhudia.

Wananchi walishiriki kazi ya kuuzima moto huo uliotokea saa 12:24 jioni. Bila kuudhibiti mapema, kulikuwa na uwezekano wa kuenea hadi nyumba za jirani kikiwemo kituo cha polisi.

“Tunawashukuru sana wananchi waliofika eneo la tukio ambao kwa kusaidiana na kikosi cha zimamoto wamefanikiwa kuuzima moto huu kabla haujaleta madhara makubwa. Kwa sasa hatuwezi kujua chanzo cha moto huu ni kipi.



“Baada ya kufanikiwa kuuzima moto huu ndiyo tutakaa na kutathimini na hili linahitaji wadau siyo polisi peke yake, kuna Kikosi cha Zimamoto na watu wengine,” alisema Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi aliyefika eneo la tukio.

Hata hiyvo, hakuna majeruhi wala aliyepoteza maisha katika tukio hilo. Pia kamanda alisema mali iliyoteketea haina thamani kubwa.

Hivi karibuni, masoko mawili jijini hapa yaliteketea kwa moto na kusababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara husika.