Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kimesema wakati huu sio muda mwafaka kujadili nani atakuwa mrithi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Zanzibar, Vuai Ali Vuai.
Akizungumza na NIPASHE katika ofisi za CCM Makao Makuu Kisiwandui Zanzibar, Vuai alisema kazi kubwa iliyopo kwa wanachama wa CCM ni kujadili utekelezaji wa ilani na sio mgombea wa urais wa mwaka 2015.
Alisema wanachama wa CCM wenye sifa za kurithi nafasi hiyo wapo wa kutosha na badala yake viongozi na wanachama watumie muda mwingi katika kutekeleza ilani ya Uchaguzi Mku wa mwaka 2010.
Alisema wakati ukifika suala la mgombea wa urais litajadiliwa na wanachama kabla ya vikao kuamua na hakuna sababu ya suala hilo kuanza kujadiliwa kabla ya muda wake.

“Wakati huu si wakujadili nani atakuwa mrithi wa Rais Kikwete, jambo la msingi wanachama na viongozi kutekeleza ilani ya uchaguzi,” alisema Vuai.
Alisema wanachama wa CCM Zanzibar na Tanzania Bara kazi yao kubwa hivi sasa ni kuimarisha chama hicho ili kiweze kuendelea kushika dola katika chaguzi zijazo.
Vuai alisema mpango wa viongozi wa CCM kujivua gamba umelenga viongozi kujirekebisha na kurudi katika misingi ya maadili ya uongozi kabla ya chama kuwafukuza watakaoshindwa kurudi katika maadili ya uongozi.
Alisema CCM inatarajia kufanya Uchaguzi wake Mkuu mwakani na kuwataka wanachama kutumia nafasi hiyo kuchagua viongoizi bora na kuwaweka kando viongozi wasio waadilifu.
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema viongozi wa CCM ambao wamekuwa na tabia ya kukosoa sera za CCM hadharani ni sawa na wasaliti ndani ya chama hicho.
“Dhambi kubwa kiongozi wa CCM kupinga sera za chama chake hadharani, huo ni usaliti ndani ya chama,” alisema Vuai.
CHANZO: NIPASHE