Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda

Serikali imeahidi kutoa tamko kuhusu taarifa za kitalaam zilizotolewa na Chama cha Madaktari nchini (MAT) kwamba dawa inayotolewa na Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapila, imeleta maafa kwa watumiaji.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda, aliyasema hayo jana alipotakiwa na NIPASHE kutoa taarifa ya serikali kuhusu kauli za MAT zilizotolewa hivi karibuni.
Katika taarifa yake, MAT ilisema wagonjwa wengi waliotumia dawa ya Babu inayotolewa kwenye kikombe, waliamua kuacha kutumia dawa zao za awali zilizotolewa hospitalini na hivyo kujikuta wakipata matatizo makubwa huku baadhi yao wakipoteza maisha.
Tangu tiba hiyo ianze kutolewa kwa maelfu ya Watanzania na wageni kutoka nje ya nchi, kumekuwepo na kauli za kupingana huku baadhi wakidai baada ya kuitumia walipona na wengine wakidai haikuwasaidia.
Dawa hiyo ambayo hadi sasa inaendelea kutolewa imeshatolewa kwa wananchi kutoka mataifa ya Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda, Oman, Uingereza, Uholanzi, Marekani,Sweeden, Malawi, Congo, Lebanon, Comoro, Zimbambwe na Malawi huku wengine wakizidi kumiminika huko.

Dk. Mponda alisema baada ya Bunge kumaliza vikao vyake, anajipanga ili kupitia taarifa ya MAT kwa lengo la kupata nafasi ya kutoa tamko la serikali kuhusu dawa hiyo.
Awali, werikali ilitoa kauli yake bungeni kuhusu dawa hiyo yaMchungaji Mwasapila kwamba haikuwa na madhara kwa watumiaji.
“Mimi nitatoa tamko la serikali baada ya kupitia taarifa hiyo ya MAT ili kuona ni kitu gani walichokuwa wakisema kuhusiana na dawa hiyo,” alisema.
Aliongeza kuwa serikali imekuwa ikifuatilia kwa karibu matumizi ya dawa hiyo na kwamba atautaarifu umma kinachoendelea kwa sasa katika tiba hiyo ya Babu.