Rais wa Ivory Coast na viongozi wengine

Ivory Coast punde itawaapisha wajumbe wa Tume ya Ukweli na Maridhiano kwa lengo la kuimarisha umoja baada ya ghasia mbaya zilizotokana na mgogoro wa uchaguzi.

Kiasi cha watu 3,000 waliuawa na wengine 500,000 kupoteza makazi yao wakati wa ghasia hizo.

Tume hiyo itaongozwa na waziri mkuu wa zamani Charles Konan Banny.

Tume hiyo ina wajumbe 11 wakiwemo viongozi wa dini, wawakilishi wa mikoa na mwanasoka maarufu wa timu ya Chelsea Didier Drogba kuzungumza na raia wa Ivory Coast waishio nje ya nchi.


Tume hiyo ina muundo sawa na ya Afrika Kusini lakini haijulikani iwapo inatoa misamaha, mwandishi wa BBC John James aliyeko mji mkuu wa Ivory, Abidjan.

Kuna masuala mengi kuhusu itakavyofanya kazi baada ya ghasia kumalizika mapema mwaka huu, anasema mwandishi wa BBC.

Usalama umeimarishwa katika maeneo mengi ya nchi na uchumi umeanza kuimarika, anaongeza.

Shirika la Fedha Duniani IMF linakisia kukua kwa uchumi kati ya asilimia 8-9 mwaka ujao.

Mashataka ya Gbagbo




Bw Ouattara alichukua madaraka mwezi April akisaidiwa na UN na majeshi ya Ufaransa baada ya kumkamata rais wa zamani Laurent Gbagbo, mjini Abidjan.

Kwa sasa anashikiliwa kaskazini mwa nchi. Yeye na mkewe, Simone, wanashtakiwa kwa uporaji, ubadhirifu, wizi wa kutumia silaha kuhusika na ghasia baada ya uchaguzi.

Bw Gbagbo alikataa kukubali kushindwa katika uchaguzi wa Novemba licha ya UN kutangaza kumtambua Bw Ouattara hasimu wake wa muda mrefu kama mshindi.