Rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy anatarajiwa kuwasili nchini Morocco kwa ajili ya uzinduzi wa ujenzi wa mtandao wa reli ya treni za mwendo kasi-TGV

Reli hiyo itaunganisha Casablanca na Rabat na Tangiers.

Makubaliano kati ya Ufaransa na Morocco kujenga reli yalisainiwa wakati Bw Sarkozy alipozuru nchi hiyo mwezi October 2007.

Bajeti ya mradi huo inakisiwa kuwa dola 4 bilioni (pauni 2.5 bilioni) na treni zitaanza kufanya kazi ifikapo mwaka 2015.

Serikali ya Morocco inasema mradi huo utaimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili. Maafisa pia wana matumaini kuwa kilometa 350 (maili 219-mile) za reli hiyo zitasaidia miundombinu.

Hata hivyo, waziri wa Fedha wa zamani nchini Morocco Mohamed Berrada anasema mradi huo ni sawa na kupoteza fedha.

Anasema fedha hizo zingeweza kutumika kwenye mambo muhimu zaidi kama kupambana na kiwango kikubwa cha umaskini na elimu duni nchini humo.

Morocco ililazimika kukopa kiasi cha dola 2 bilioni kutoka benki za Ufaransa na mifuko ya fedha ya maendeleo kutoka Saudi Arabia kwa ajili ya mrdai huo.

Kwa mujibu wa Karim Tazi, mtaalam wa jamii kiasi kilichoasalia cha fedha zilizokopwa hakina budi kulipwa na vizazi vijavyo.

Baadhi ya wachambuzi wanahoji iwapo kweli kuna umuhimu wa Morocco kujitosa kwenye madeni zaidi kwa lengo la kupunguza muda wa safari kati ya Tangiers na Casablanca kutoka saa 5 hadi saa mbili na dakika kumi.