Umoja wa Afrika (AU) umesema unatarajia kupokea majeshi ya ziada 3,000 katika kipindi cha miezi sita ijayo kuongeza nguvu katika shughuli zake Somalia.
Lt Kanali Paddy Ankunda, msemaji wa jeshi la AU Somalia, alisema majeshi yatatoka Djibouti na Sierra Leone.
Kwa sasa AU ina takriban askari 9,000 kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Makamanda wa AU kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamika kuwa hawana askari wa kutosha.
Usambazaji wa majeshi yao kwa sasa ni ndogo sana kuweza kudhibiti mji mzima, licha ya wapiganaji wa al-Shabab kuondoka baadhi ya sehemu waliokuwa wameshikilia mpaka mapema mwezi Agosti.
Kufuatia kurudi nyuma kwao, kamanda mkuu wa AU nchini Somalia, Meja Jenerali Fred Mugisha, alitaka maelfu ya majeshi ya ziada kuweka usalama kwenye mji mkuu huo.
Lakini licha ya viongozi wengi wa Afrika kutoa ahadi ya maneno matupu, Uganda na Burundi pekee ndizo zimejiandaa kutoa askari katika harakati hizo za hatari.
0 Comments