Wachezaji wa timu ya Taifa ya netiboli 'Taifa Queens' wakiwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam jana wakitokea Maputo, Msumbiji walikotwaa medali ya fedha katika mashindano ya All Africa Games. (Na Mpigapicha Wetu).
SERIKALI imesema itaendelea kuhamasisha maendeleo ya mchezo wa netiboli kwa kutafutia udhamini ikiwa pamoja na kushiriki kikamilifu kuuendeleza.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emanuel Nchimbi wakati wa kuipokea timu ya Taifa ya netiboli ‘Taifa Queens’ iliyorejea nchini
ikitokea Maputo, Msumbiji ilikotwaa medali ya fedha katika michezo ya All Africa Games.
Alisema Taifa Queens wanastahili pongezi kwa kuwa wameliletea sifa kubwa taifa na kwamba wizara yake imeona ni kweli timu hiyo inastahili msaada wa hali na mali.
Alieleza kuwa kumekuwa na visingizio vingi likiwamo suala zima la ukosefu wa vifaa vya michezo, lakini vifaa hivyo vilikuwapo kulingana na mahitaji yaliyotakiwa.
Taifa Queens ilirejea jana mchana pamoja na timu ya Taifa ya soka ya wanawake‘Twiga Stars’, ambayo haikufanya vizuri.
Taifa Queens imemaliza mashindano hayo yaliyoshirikisha timu tisa upande wa netiboli baada ya kufikisha pointi 12 sawa na Zambia iliyotwaa medali ya shaba, lakini Taifa Queens ilikuwa na mabao mengi ya kufunga, hivyo kushika nafasi ya pili nyuma ya Uganda iliyotwaa medali ya dhahabu.
Taifa Queen imecheza michezo nane, imeshinda sita na kupoteza miwili. Mwaka 2007 katika mashindano kama hayo yaliyofanyika Algiers, Algeria, Tanzania ilipata medali moja ya
fedha iliyonyakuliwa na Martine Sulle katika mbio za nusu Marathon. Source Habari Leo.
0 Comments