Kumekuwa na milolongo mirefu nje ya vituo vya kupigia kura wakati huu Wazambia wanapiga kura katika kile kinachotarajiwa kuwa kinyanganyiro kikali zaidi katika historia ya uchaguzi nchini Zambia.
Kumekuwa na taarifa za kuchelewa kwa shughuli hiyo na vile vile ghasia lakini wachunguzi wa uchaguzi wanasema utaratibu mzima wa upigaji kura umekuwa mzuri hadi sasa.
Rais Rupiah Banda anatarajiwa kukabiliana na mpinzani wake mkubwa Michael Sata.
Tangu uchaguzi wa mwaka 2008, watu wengine, ikiwa ni zaidi ya milioni moja wamejiandikisha kuwa wapigaji kura ,wengi wao ni vijana ambao hawana ajira.
Bei ya juu ya madini ya shaba imeimarisha ukuaji wa uchumi wa Zambia lakini wananchi wa kawaida wanasema hawajapata faida yoyote kutokana na ukuaji huo.
Maelfu ya Polisi wamepelekwa sehemu mbalimbali ilikuepusha ghasia na uuzaji wa shoka na vifaa vingine ambavyo vinauwezo wa kutumika kama silaha umepigwa marufuku katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Rais Banda alimshinda Sata kwa kura 35,000 katika uchaguzi wa mwaka 2008, ulioitishwa baada ya kifo cha Rais Levy Mwanawasa, hii ilisababisha ghasia kubwa ambazo zilizochochewa na baadhi ya wafuasi wa upinzani katika ngome zao za mijini .
Watu milioni 5.2 wanatarajiwa kupiga kura, hii ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya watu waliojiandikisha kuwa wapiga kura katika uchaguzi huu wa Rais, wabunge na waakilishi wa serikali za mitaa.
Upigaji kura ulianza saa kumi na mbili asubuhi saa za Zambia na utamalizika saa kumi na mbili jioni ambapo matokeo ya mwanzo yanatarajiwa Jumatano jioni.
Wizi wa kura
Shirika la habari la AFP limezungumzia ghasia katika kituo kimoja cha kupigia kura mjini Lusaka ambako yasemekana wafuasi wa upinzani wamempiga mtu mmoja ambaye inaaminika alikuwa amebeba karatasi ya kupigia kura ambayo ilikuwa tayari imeshatiwa alama.
Baadae wafuasi hao waliivurumishia mawe picha ya kampeini ya Rais Banda na kuweka vizuwizi katika barabara zinazoelekea Kanyama kitongoji kimoja cha mabanda.
Baadhi ya vituo kadhaa vya kupigia kura inasemekana vilianza shughuli zake kuchelewa kutokana na upungufu wa vifaa vya kupigia kura.
0 Comments