Hatimaye mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya kutorosha aina 14 za wanyama pori hai 136 na ndege vyennye thamani ya Sh. milioni 170, Kamran Ahmed (29), amerejea nchini baada ya kupewa ruhusa ya kwenda kwao Pakistan, hatua iliyozua uvumi kuwa hatarejea kutokana na kesi inayomkabili.
Kamran anadaiwa kuripoti katika ofisi za Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Moshi na Polisi baada ya kurejea.
Kwa mujibu wa taarifa za uhakika zilizopatikana mjini hapa na kuthibitishwa na mmoja wa watumishi wa Mahakama Kuu ambaye hakutaka kutaja jina lake kwa kuwa si msemaji, Kamran alipokelewa kwa furaha na baadhi ya watumishi wa Mahakama kufuatia wasiwasi uliozuka kuwa asingerejea.
“Leo ilikuwa kama sherehe, mshtakiwa wa kesi ya twiga karudi, kafika hapa mahakamani kuuliza hati ya kusafiria airudishe polisi au mahakamani, yaani alipokelewa kama shujaa maana hali ilishakuwa mbaya kwa Hakimu Mfawidhi, Simon Kobelo, ambaye ndiye alimpa ruhusa hiyo,” alisema.

Habari kutoka mahakamani zinadai kuwa mshtakiwa huyo alipewa ruhusa ya siku 15 na kutakiwa kurejea Septemba 14, mwaka huu, ambapo kesi dhidi yake na wenzake inatarajia kutajwa Septemba 30, mwaka huu.
Kobelo ambaye alikuwa kaimu Msajili wa Mahakama Kuu tangu aliyekuwa Msajili, Aron Lyamuya, kuhamishiwa Mbeya, alithibitisha mshtakiwa huyo kupewa ruhusa ya siku 15.
Kabla ya Kamran kurejea nchini, Msajili wa Mahakama Kuu, Amosi Fungo aliiambia NIPASHE kuwa hakuwa na taarifa zozote kuhusiana na mshtakiwa huyo kupewa ruhusa kwa maelezo kuwa ana siku mbili tangu aalipohamishiwa kwenye ofisi hiyo.
Mshitakiwa huyo na wengine wapo nje kwa dhamana iliyotolewa na jaji Moses Mzuna ikiwa na masharti sita ikiwa ni pamoja na kila mshtakiwa anatakiwa kukabidhi mahakamani Sh. milioni 14.2 au mali yenye thamani hiyo.
CHANZO: NIPASHE