Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willbroad Slaa, alisema hayo kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Urughu, wilayani Iramba, Mkoa wa Singida, baada ya wananchi kulalamika kuwa katika kijiji cha Urughu na eneo lote la kata hiyo, huchangishwa kila kaya Sh. 25,000 bila kupewa risiti.
“Nimeambia mnachangishwa Shilingi 25,000 kila kaya, tena bila kupewa risiti, kweli si kweli?” alihoji na kuongeza: “Kupokea fedha ya Mtanzania bila risti ni wizi. Nawaomba sana akija mtu kukuchangisha mwambie nipe risiti…bila risiti, ripoti polisi akamatwe pale pale.”
Dk. Slaa alisema chini ya sheria na utawala bora, endapo wananachi watabaini mtendaji wa kijiji hatendi haki, ikiwemo kutosoma taarifa ya mapato na matumizi, wanaweza kuitisha mkutano mkuu kwa kumtumia kiongozi wa eneo lingine na kumkataa mtendaji huyo.
“Ndiyo maana sisi wapinzani tunachukiwa kwa sababu tunawaelimisheni sana, mkiona mtendaji anawasumbua, hawasomei taarifa ya mapato na matumizi, amekula hela zenu, anawanyanyasa kwa michango isiyo na risiti mkataeni,” alisema huku akishangiliwa.
Kwa mujibu wa Dk.Slaa Mkutano Mkuu unaitishwa kwa kufuata kifungu cha 146 cha sheria namba saba ya mwaka 1982, amacho kinabainisha wazi kuwa endapo mtendaji hatakiwi kwenye eneo husika, anatakiwa kutolewa mara moja, badala ya kumsubiri mkurugenzi mtendaji wa halmashauri.
“Kifungu cha sheria namba 146 kinasema kuwa wananchi ndiyo wanaoiweka madarakani serikali ya kijiji na ndio wenye mamlaka ya kuiondoa madarakani endapo haitakuwa tayari kuwatumikia na hakuna mahali popote duniani pa kwenda kukata rufaa,” alisistiza Dk. Slaa.
Mbunge wa viti Maalumu (Chadema), Christowaja Mtinda, aliwaomba wananchi kumchagua mgombea wa chama hicho, Fanueli Kitundu, ili aweze kuwaletea maendeleo.
CHANZO: NIPASHE
0 Comments