Majeshi ya Amisom

Wanajeshi wa Muungano wa Afrika wanasema wamewafurusha wapiganaji wa al-Shabab kutoka ngome yao ya mwisho kaskazini mwa mji mkuu wa Somali Mogadishu.

"Sasa tunaudhibiti mji mzima wa Mogadishu" Jenerali Fred Mugisha wa kikosi cha Muungano wa Afrika amesema na kuongeza kuwa vikosi vya serikali ya Somalia vilishiriki katika mashambulizi hayo.
Mwanajeshi mmoja wa Muungano wa Afrika na raia wanane waliuawa katika mapigano hayo.

Al-Shabab bado inadhibiti maeneo makubwa ya kusini na Somalia ya Kati.


Jenerali Mugisha amenukuliwa na BBC akisema,"Vikosi vya serikali ya mpito ya Somalia vikiungwa mkono na kikosi cha kudumisha amani cha Muungano wa Afrika tumeweza kuwafurusha al-Shabab kutoka mji mkuu wa Mogadishu, wakati huu ninapozungumza tunaudhibiti kabisa mji wa Mogadishu".

Msemaji wa Amisom Luteni Kanali Paddy Ankunda amesema kuwa lengo lilikuwa kuwaondoa al-Shabab nje karibu na raia.

"Maeneo ya nje ya kaskazini na mashariki ya mji huo lazima yasafishwe kabisa lakini maeneo na majengo muhimu kwa sasa hayako tena chini ya udhibiti wa wanamgambo wa kiislamu" aliongeza msemaji wa Amisom.

Luteni Kanali Ankunda aliongeza kuwa kiwanda kimoja cha kutengeneza pasta kilichokuwa kinatumiwa na al-Shabab kama kituo chao kikuu cha operesheni zake kimekamatwa.

Mwandishi wa BBC aliye Mogadishu anasema bado kuna wanamgambo wa al-Shabab katika wilaya ya Daynile.

Al-Shabab walisema kuwa walihusika na shambulio la bomu la wiki jana lililosababisha vifo vya watu 80.

Kundi hilo lenye uhusiano na al-Qaeda liliondoka kutoka sehemu kadhaa za Mogadishu mwezi Agosti kufuatia mashambulizi ya Amisom, lakini wadadisi wameamua kuwa bila ya kuwa na wapiganaji katika mstari wa mbele wa mapambano, kuna uwezekano wa kundi hilo kufanya mashambulizi zaidi ya bomu ikiwa nipamoja na yale ya kujitoa mhanga.