Aliyekuwa jasusi mkuu wa Kanali Maummar Gaddafi aliyekimbilia Uingereza mwezi Machi, binafsi aliwatesa wafungwa wa kisiasa Libya, kipindi cha BBC Panorama kimeambiwa.

Moussa Koussa alikuwa mshirika mkubwa wa aliyekuwa kiongozi huyo na kiunganishi kikuu wa shirika la kijasusi la Uingereza baada ya shambulio la Septemba 11 wakati Libya ilipoanza kutafuta washirika wapya.
Ameshutumiwa pia kuhusika na shambulio la bomu la Lockerbie mwaka 1998.

BBC ilimsaka Bw Kousaa kwenye hoteli ya kifahari nchini Qatar lakini alikataa kujibu lolote kuhusu madai hayo mapya.

Nchini Libya, Muftah Al Thawadi alikiambia kipindi hicho kwamba binafsi aliteswa na Bw Koussa mwaka 1996 katika gereza kubwa sana mjini Tripoli liitwalo Abu Salim.

"Wakati nilipokuwa nikihojiwa, Mousaa Koussa alikuwa akinitesa kwa kunichoma na umeme shingoni kwa kutumia nyaya za umeme," alielezea alipokuwa akihojiwa.

Utekaji nyara, kuwahamisha kisiri washukiwa


Katika miaka ya hivi karibuni, Moussa Koussa alikuwa kiungo muhimu katika majadiliano na mashirika ya kijasusi ya Uingereza na Marekani kuhusu hatua ya Libya kulaani ugaidi na kuachana na silaha zake za maangamizi.

Baada ya kuporomoka kwa mji wa Tripoli mwezi Septemba, wafanyakazi kutoka shirika la Human Rights Watch waligundua nyaraka katika iliyokuwa ofisi ya Moussa Koussa zilizoonyesha kiwango cha ukaribu alionao na mashirika ya kijasusi ya kigeni yakihusihwa na vita dhidi ya ugaidi.


Nyaraka hizo zilionyesha taarifa za utekaji nyara na kuhamishwa kisiri kwa washukiwa wa ugaidi.

Ugunduzi huo kulisababisha waziri mkuu wa Uingereza David Cameron kuwasilisha taarifa hizo kwenye uchunguzi wa waliotiwa kizuizini na kutangazwa kwa mara ya kwanza Julai 2010 ili kutathmini iwapo mamlaka ya Uingereza " ilihusishwa na kuwatesa, au kuwasafirisha kisiri, waliotiwa kizuizini na nchi nyingine katika harakati za kupambana na ugaidi nje ya nchi" baada ya shambulio la Septemba 11.

Bw Thawadi alisema, kwa upande wa Moussa Koussa, umefika wakati wa serikali za kimagahribi kutambua ni mtu gani waliyekuwa wakifanya naye biashara na kumlazimisha akabiliane na sheria.

"Ni mwuaji na mhalifu na alichojali ni uongozi huu uliojaa ufisadi ulioitawala Libya kwa chuma na moto ili uendelee kuwepo madarakani. Mousaa Koussa alitesa watu.