Kumezuka hofu kwamba viongozi wa Ulaya huenda watashindwa kuafikiana suluhu la tatizo la madeni linalotishia kusambaratisha uchumi wa bara hilo.
Viongozi hawa wanakutana mjini Brussels, Ubelgiji kwa kikao ambacho wanasema kitatatua matatizo hayo.
Ni mkutano wa pili katika kipindi cha siku nne.
Agenda kuu ni kwa kiwango gani deni la serikali ya Ugiriki katika taasisi za kibinafsi litafutwa na iwapo mfuko wa mkopo wa dhamana wa muungano wa Ulaya unafaa kuongezewa fedha.
Hata hivyo kiongozi wa vyama vyenye msimamo wa kadri katika bunge la ulaya Guy Verhofstadt, ameiambia BBC kuwa hana imani kwamba maafikiano ya leo yatasaidia kurejesha uthabiti katika sekta ya fedha barani Ulaya.
"Ni wazi kuwa lazima tuongeze fedha katika hazina ya kukomboa uchumi wa Ulaya, hiyo itasaidia mataifa mengi yanayokabiliwa na wakati mgumu wa kifedha. Lakini kuna wasiwasi ya masoko ya ulaya kwamba hayataonelea hii kama hatua mwafaka kwa hivyo wengi wanahofia kwamba badala ya kutafuta suluhu la kudumu tunaangazia suluhisho za muda tu." alisema Verhofstadt.
0 Comments