SHESHE la kufungiwa kushiriki katika filamu kwa nyota mwenye mvuto runingani, Aunt Ezekiel ‘Gwantwa’, limepandisha juu presha za baadhi ya mastaa wa kike ambao wanadai kuwa amefanyiwa kitu kibaya, The Biggest IQ paper, Ijumaa Wikienda lina data nzito.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, mastaa hao walishtushwa na kitendo cha Aunt kufungiwa kuigiza kwa miezi minne eti kisa kikidaiwa ni nyodo na mengine yaliyo nyuma ya pazia (tunayafanyia kazi, tega sikio kwenye magazeti pendwa ya Global Publishers).
Wa kwanza kubwabwaja alikuwa ni staa wa filamu aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa kuogopa naye kupigwa ‘stop’ kuonekana kwenye runinga, ambaye alisema kuwa watu wanalichukulia suala la kufungiwa kwa Aunt kwa wepesi lakini nyuma yake kuna kitu kikubwa kimejificha.
Staa huyo alisema rungu lililomshukia Aunt linanukia kwa mastaa wengine kama Wema Sepetu (pichani), Irene Uwoya, Jacqueline Wolper, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na wengine wa kike katika tasnia hiyo.
“Nyie endeleeni na uchunguzi wenu, mtagundua kuwa kuna kitu kizito na mkikiweka hadharani hakutakuwa na Bongo Movie tena, kiukweli sakata la Aunt ni kubwa na siyo la kuliangalia kwa juu juu tu,” alisema staa huyo.
Ijumaa Wikienda liliwatafuta mastaa wengine wa kike wenye majina makubwa katika fani ya filamu ambao wanadaiwa muda si mrefu yatawakuta yaliyompata Aunt.
ELIZABETH MICHAEL ‘LULU’:
“Kiukweli sina cha kuzungumza kwani kama unavyojua tatizo lenyewe halijawekwa wazi, kila mtu anasema lake, binafsi naomba viongozi wamsamehe kwani ni tukio la kwanza, kisha watuweke wazi na sisi ili tusifike huko tukajikuta tukifungiwa.”
WEMA ISAAC SEPETU:
“Sikupenda kabisa kitu alichofanywa Aunt, kusema kweli Bongo Movie kuna watu wanaojiona ni miungu watu, kuna vitu vingi vinafanyika siye tunakaa kimya, kila mtu pale ana ‘mashauzi’ yake, hakuna umoja, mtu anakaa kumtengenezea mwenziye majungu, kwa sasa siwezi kupoteza muda kwenda kukaa Leaders (klabu) kwa ajili ya kunywa pombe tu, ila kama kuna kitu cha maana nitakwenda, mimi sina nyodo na natambua kuwa bosi wangu ni Steps Entertainment, hivyo hawawezi kunifungia hata siku moja.”
JACQUELINE WOLPER:
“Duh! Kwanza nilishtuka kwa kuwa sikuwepo kwenye vikao, sijui chochote kuhusiana na chanzo cha kufungiwa kwa Aunt lakini inaniuma sana kwa sababu filamu ndiyo kazi zetu zinazotuweka mjini.”
IRENE UWOYA
Ijumaa Wikienda lilipomtafuta Uwoya ambaye mwaka jana naye alipatwa na kimbembe cha kufungiwa ili kupata maoni yake, halikufanikiwa kwani simu yake haikuwa hewani kila ilipopigwa.
STEPS WANASEMAJE?
Akizungumzia ishu hiyo, Afisa Uhusiano wa Steps Entertainment, Seles Mapunda alisema tangu wapokee taarifa ya kufungiwa kwa Aunt na kutoa ushauri wao kuwa aonywe mambo yaishe hawajapokea taarifa nyingine juu ya ishu hiyo.
AUNT HAYUPO TAYARI KUSEMA CHOCHOTE
Aunt alifungiwa na viongozi wa Bongo Movie kushiriki katika filamu kwa miezi minne ambapo hakuwa tayari kuweka wazi ‘sosi’ ya ishu hiyo.
(global publishers).
0 Comments