Mawaziri watatu wa ngazi za juu wametangaza kujiuzulu kutoa nafasi uchunguzi ufanywe kuhusu madai ya ufisadi dhidi yao, hatua hii imetokea baada ya bunge la Uganda kupiga kura kusitisha mipango yote mipya ya biashara katika sekta ya mafuta, hii inafuatia madai kuwa mawaziri wa serikali wamekuwa wakipokea rushwa ya mamilioni ya dollar kutoa kandarasi hizo za mafuta Uganda.

Mawaziri hao ni Sam Kutesa Waziri wa Mambo ya Nje; Kiranja Mkuuu wa upande wa serikali John Nasasira,ambae kwa muda mrefu aliwahi kuwa Waziri wa Usafiri na Waziri Mdogo wa Kazi Mwesigwa Rukutana.
Mbunge Gerald Karuhanga siku Jumatatu aliliambia bunge kuwa kampuni ya Uingereza ya Tullow ilitoa rushwa ili kuwa na ushawishi katika maamuzi.

Tullow kwa upande wake imekatalia mbali madai hayo ikisema ni uzushi mtupu.

Wadadisi wanasema kura hii ni pigo kubwa kwa Rais Yoweri Museveni ambaye amekuwa mamlakani tangu mwaka 1986.

Mwandishi wa BBC Joshua Mmali akiwa katika mji mkuu wa Uganda, Kampala anasema hii ina maana serikali haitaweza kutia saini makubaliano mapya ya mafuta hadi pale sheria kuhusu petroli itakapoundwa.

Katika mjadala mkali siku ya Jumatatu, Bw. Karuhanga alionesha nyaraka zilizodai kuwa kampuni ya Tullow ilimhonga Waziri Mkuu Amama Mbabazi, Waziri wa Mshauri ya Kigeni Sam Kutesa na aliyekuwa Waziri wa Nishati Hilary Onek

Bw. Hilary Onek ambaye ameshutumiwa kupokea Euro milioni 17 amekanusha vikali madai hayo.


"Kwa kweli uwongo huu umenipa machungu mengi kwa kuwa ikiwa kama nina akaunti kama hiyo basi ninafaa kupata kila adhabu iliyopo duniani" Bw. Onek aliwaambia wabunge.

Kwa upande wake kampuni ya Tullow imesema itafurahia kufika mbele ya kikao chochote kile kukanusha madai haya.

Bw. Kutesa amemshutumu Bw.Karuhanga kwa kutumia vibaya fursa yanayopewa na bunge kwa kutoa madai ya uwongo.

"Je anafaa kweli kutoa matamshi mbaya kama haya ya kunichafua jina taarifa ambazo ni za uwongo ambazo anajua waziwazi hawezi kuzitoa nje ya jengo la bunge?" aliuliza Bw. Kutesa.

Bw. Karuhanga alijibu kuwa yuko tayari kurudia madai hayo hata nje ya bunge.

Bw. Mbabazi aliisoma barua kwa wabunge kutoka mkuu wa kampuni hiyo ya Tullow Aidan Heavey.

"Madai haya ni ya uwongo na inaonesha yametolewa kutokana na kutoelewa jinsi shughuli za biashara ya mafuta na gesi ulimwenguni zinavyoendeshwa" barua ilieleza.

Mwandishi wetu anasema kuwa wabunge wametaka kuwe na uwazi zaidi katika sekta ya mafuta na kuitaka serikali kufichua maelezo ya kile walikiita mipango ya siri na kampuni ya mafuta ya Tullow.

Waandishi wanasema kuwa kura hiyo ambayo pia iliungwa mkono na wabunge kutoka chama tawala inaonesha kuwa ushawishi wa Rais Museveni kwa wabunge wake umeanza kulegea.
.


"