Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura kumaliza harakati zake za kimataifa za kijeshi nchini Libya kuanzia Jumatatu ijayo.
Mwezi Machi baraza hilo lilipiga kura kuidhinisha " hatua zote muhimu" kuwalinda raia, baada ya aliyekuwa kiongozi Muammar Gaddafi kuanzisha mashambulio kwa waandamanaji waliopinga uongozi wake.
Wiki iliyopita majeshi ya Nato na washirika wake, ambao walikuwa wakifanya mashambulio ya anga, wamesema harakati zao zitamalizika Oktoba 31.
Serikali mpya ya Libya ilitangaza nchi hiyo kukombolewa siku ya Jumapili.
Siku ya Alhamisi baraza hilo lilipitisha azimio kumaliza makubaliano ya harakati za kijeshi kutoka nchi za kigeni Oktoba 31.
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague alisema kura hiyo ilikuwa "mafanikio kuelekea hatima ya Libya katika misingi ya amani na demokrasia".
'Harakati zafanikiwa'
Azimio hilo lilitolewa licha ya wito kutoka kwa baraza la mpito la taifa la Libya NTC kutaka Nato kuendelea na harakati zake za kijeshi.
Ujumbe wa Libya kwenye umoja wa mataifa ulisema NTC ulihitaji muda zaidi kutathmini mahitaji yake ya kiusalama.
Lakini wanadiplomasia wa baraza la usalama waliwaambia waandishi wa habari kuwa makubaliano ya kulinda raia yamefanikiwa, na msaada wowote wa ziada wa usalama lazima ujadiliwe katika makubaliano tofauti.
Wakati wa harakati zao za miezi saba nchini Libya, muungano huo umefanya mashambulio takriban 36,000 ya ndege.
Waandishi wamesema harakati hizo zimekuwa na umuhimu sana katika jitihada ya kumwondoa Kanali Muammar Gaddafi, aliyoendolewa Agosti na kuuawa wiki iliyopita.
Urusi, China, Afrika Kusini, India na Brazil zilipinga vikali mashambulio hayo, na kuishutumu Nato kwa kukiuka makubaliano ya umoja wa mataifa.
Lakini siku ya Alhamisi ujumbe wa Marekani kwa umoja wa mataifa, Susan Rice, alisema historia itachukulia uvamizi huo kama "jambo la kujivunia tangu kuwepo kwa Baraza la Usalama".
0 Comments