Watu wenye silaha nchini Kenya wameshambulia lori la mizigo karibu na mpaka na Somalia, na kuua watu wasiopungua wanne.

Taarifa zinasema gari hilo lilikuwa limebeba makaratasi ya mitihani ya shule, wakati liliposhambuliwa katika wilaya ya Mandera.
Kenya inalaumu kundi la wanamgambo la al-Shabaab kwa mfululizo wa utekaji nyara katika ardhi yake.
Vifo
Al-Shabaab inakanusha tuhuma hizo na imeahidi kulipiza kisasi kwa Kenya kwa kupeleka majeshi yake nchini Somalia.

Msemaji wa shirika la Msalaba Mwekundu Nelly Muluka-Oluoch ameliambia shirika la habari la AFP kuwa wafanyakazi wa shirika lake waliokwenda katika eneo la tukio wameripoti vifo vya watu wanne.

Washambuliaji hao walifyatua risasi na mabomu katika gari hilo, ambalo lilikuwa limebeba makaratasi ya mitihani, limesema shirika la habari la AP.


Abiria


Msemaji wa polisi wa Kenya, Erick Kiraithe ameelezea shambulio hilo kuwa la "kijambazi". Shirika la habari la Reuters limesema shambulio hilo limetokea kilomita 110 kutoka mji wa Mandera.

Msemaji wa polisi pia amesema baadhi ya maafisa wa serikali walikuwa abiria ndani ya gari hilo.

Kenya ilituma mamia ya wanajeshi nchini Somalia Oktoba 16 kuwasaka al-Shabaab ambao wanadhaniwa kuwa na uhusiano na kundi la al-Qaeda.

Al-Shabaab imekuwa ikitishia mara kwa mara kufanya mashambulio ya kulipiza kisasi kwa Kenya.

Milipuko


Siku ya Jumatano, mtu mmoja kutoka Kenya aliyekamatwa kuhusiana na milipuko ya mabomu mjini Nairobi, alikiri mahakamani kuwa mwanachama wa kundi hilo.

Elgiva Bwire Oliacha alikiri kufanya mashambulio katika klabu ya starehe na katika kituo cha basi.

Mtu mmoja aliuawa na wengine 29 kujeruhiwa katika mashambulio ya Oktoba 24.

Usalama umeimarishwa mjini Nairobi tangu kutokea kwa mashambulio hayo, huku wakazi wengi wakihofu kuwa huenda kukawa na mashambulio zaidi, wanasema waandishi wa habari.Wiki iliyopita, mamlaka za Ufaransa zilisema mwanamke mmoja raia wa Ufaransa anayeugua saratani alitekwa nyara kutoka Kenya na Wasomali wenye bunduki mapema mwanzoni mwa mwezi alifariki dunia.
Raia wengine wa kigeni waliotekwa kutoka Kenya na kushikiliwa nchini Somalia ni pamoja na mwanamke mmoja raia wa Uingereza aliyetekwa nyara kutoka katika hoteli moja kwenye mwambao wa Kenya, dereva mmoja raia wa Kenya na wafanyakazi wawili wa utoaji misaada raia wa Uhispania waliotekwa kutoka kambi ya wakimbizi ya Daadab iliyopo karibu na mpaka kati ya Kenya na Somalia.