Watu 36 miongoni mwa waliojeruhiwa sana katika shambulio la kujitoa mhanga siku ya Jumanne kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, wanapelekwa Uturuki kwa matibabu.

Miongoni mwa waliopelekwa ni vijana ambao kwa wakati wa mlipuko huo walikuwa kwenye wizara ya elimu kuona iwapo wameshinda mssada wa masomo kwenda Uturuki.

Kundi la wanamgambo la al-Shabab lilisema lilifanya shambulio hilo.

Takriban watu 150 walijeruhiwa na 77 wamefariki dunia baada ya lori kulipuka nje ya majengo mengi ya wizara za serikali.

Ni shambulio kubwa kutokea tangu al-Shabab kuondoa majeshi yake Mogadishu mwezi Agosti.

Walioathirika kwa moto

Waziri mkuu wa Uturuki alitembelea Somalia hivi karibuni na kuahidi kutoa msaada kwa nchi hiyo iliyoathirika na vita.


Mwandishi wa BBC Mohammed Moalimu mjini Mogadishu alisema wagonjwa 37 walipelekwa uwanja wa ndege wa Mogadishu Alhamis aubuhi, lakini mmoja alifariki dunia kabla hata ya ndege kuondoka.

Waziri wa sheria wa Somalia Ahmed Bile, ambaye ni mkuu wa kamati maalum iliyoundwa kushughulikia yaliyojiri baada ya shambulio hilo, alisema wengi waliopelekwa na ndege Uturuki ni wale walioungua sana.

Mwandishi wetu alisema hospitali kuu ya Mogadishu imekuwa ikipata tabu kuwashughulikia waliojeruhiwa.

Baadhi ya watu walikuwa wamelala nje wakipata matibabu baada ya Rais Sheikh Sharif Sheikh Ahmed alipotembelea siku ya Jumatano, siku moja baada ya mlipuko.

Alitangaza mfuko wenye thamani ya dola za kimarekani 100,000 umeundwa kuwatibu walioathirika na kuwasaidia ndugu wa wafiwa.