NDOA na iheshimiwe na watu wote! Wakati mwanamitindo maarufu Bongo, Jacqueline Patrick (pichani), akijiandaa kuolewa Novemba, mwaka huu, baadhi ya ‘washakunaku’ wameanza kuivunjia heshima ndoa yake kwa kutia shaka kama kweli ataweza kutulia au la, Amani pekee ndilo lenye mkanda mzima.
Kwa mujibu wa chanzo makini, miguno na minong’ono ilisikika mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kikao cha maandalizi ya ndoa hiyo ambapo baadhi ya wadau wa sanaa na rafiki wa karibu wa mwanamitindo huyo walionesha kuingiwa na hofu.
Chanzo hicho kilitambaa na mistari kuwa kinachomponza Jack ni mwonekano wake katika jamii wa kupenda kujiachia kihasara kwa vivazi vya mitego pamoja na kupenda starehe kama ilivyo kwa mastaa wengine walioshindwa kudumu katika ndoa zao.NUKUU
Nukuu za wadau hao zilikuwa hivi: “Je, Jack ataweza kutulia kwenye ndoa? Je, ataweza kuachana na mashoga zake ambao ni micharuko? Je, ataondoaje kumbukumbu za matukio mabaya? Na kama akishindwa, je, mumewe atawezaje kuvumilia skendo zitazoiandama ndoa yao?”
Ilisemekana kuwa kama Jack hatabadilika na kuacha mambo au tabia zisizoendana na maadili ya ndoa, nyumba itamshinda ndani ya kipindi kifupi.
JACK ANASEMA?
Baada ya kusikia maneno ya ‘washakunaku’ wa mambo ya watu, Amani lilimuinulia mkonga wa simu na kumsomea mkanda mzima wa kile kinachosemwa mtaani kisha kutaka kujua amejiandaaje kukabiliana na maoni hayo ya wadau na ndugu zake katika maisha ya ndoa.
Jack ambaye ni Miss Ilala namba 3, 2005 alianza kwa kusema kuwa hadi kufikia kuchukua hatua ya kuolewa amefanya uamuzi sahihi uliyotoka moyoni mwake na wala hakukurupuka kama wengi wanavyodhani.“Nimeamua kwa hiyari yangu kuolewa na sijafanya hivyo kwa fasheni, nimepima jinsi ninavyoweza kuishi na mume wangu kwa raha mustarehe,” alisema Jack.
ETI KAPENDA KUTOKA MOYONI
Mrembo huyo ‘seksi’ aliongeza kuwa mwanaume anayetaka kumuoa ni mstaarabu na anayefaa kuwa mume wa mtu ambaye amempenda kutoka moyoni mwake.
“Nilijua watu watahoji kuhusiana na ndoa yangu, lakini nina heshima na nitawashangaza wengi, nawaomba waniombee mema tu wala wasinichukulie nilivyo kwani siko hivyo,” alisema Jack ambaye bado hakuwa tayari kumwanika mumewe mtarajiwa.
NI KINARA WA PICHA ZA NUSU UTUPU
Jack ambaye ni kinara wa picha za nusu utupu mtandaoni, aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na aliyekuwa mtoto wa Mbunge wa Koani, Mafia, Haroub Masoud, Ifraji Haroub ambapo walitengana kwa maneno mbofumbofu huku mnyange huyo akiambulia kipigo ‘hevi’.
0 Comments