Mkurugenzi Mtendaji wa Ewura, Haruna Masebu.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (Ewura), imetangaza bei mpya za aina zote za mafuta za jumla na rejareja zitakazoanza kutumika kuanzia leo, huku bei za petroli zikishuka na bei za dizeli na mafuta ya taa zikipanda.
“Ewura inatangaza bei elekezi na bei kikomo za mafuta ya petroli hapa nchini. Bei hizi zitaanza kutumika kuanzia Jumatatu, tarehe 10 Oktoba 2011,” alisema Anastas Mbawala kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Ewura, Haruna Masebu.
Kwa mujibu wa Mbawala, katika mabadiliko hayo, bei ya petroli imeshuka kwa Sh. 38.35 kwa lita, sawa na asilimia 1.82, wakati bei ya dizeli imepanda kwa Sh. 16.95 kwa lita (asilimia 0.85) na bei ya mafuta ya taa imepanda kwa Sh. 9.35 kwa lita (asilimia 0.48).
Mbawala alisema mabadiliko hayo ya bei za mafuta, yametokana na sababu kuu mbili; ya kwanza ikiwa ni kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
Sababu ya pili, ni kutokana na kushuka kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola ya Marekani, ambayo hutumika katika manunuzi ya bidhaa za mafuta katika soko la dunia.
Mbawala alisema bei za aina zote za mafuta zingeshuka kama thamani ya shilingi isingeendelea kushuka ikilinganishwa na dola ya Marekani.
Alisema kwa kulinganisha toleo la sasa na toleo lililopita, thamani ya shilingi katika toleo la sasa imepungua kwa asilimia 1.96.
Mbawala alisema bei za jumla kwa kulinganisha matoleo hayo mawili, zimebadilika, ambapo petroli imeshuka kwa Sh. 38.36 kwa lita (asilimia 1.89). Alisema bei ya dizeli imepanda kwa Sh. 16.95 kwa lita (asilimia 0.88) wakati bei ya mafuta ya taa imepanda kwa Sh. 9.37 kwa lita (asilimia 0.49).

Mbawala alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya petroli, zitaendelea kupangwa na soko na kwamba, Ewura itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa hizo.
Alisema taarifa hizo zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta. Hata hivyo, alisema kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo kama ilivyokokotolewa na fomula iliyopitishwa na Ewura na ambayo ilichapwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 5 la Januari 9, mwaka juzi na marekebisho yaliyofanywa kupitia Tangazo la Serikali Na. 216 la Julai 29, mwaka huu.
Alivitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionyesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika.
Pia aliwashauri wateja kununua bidhaa za mafuta kutoka kwenye vituo vinavyouza mafuta kwa bei ndogo zaidi ili kushamirisha ushindani.
“Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja na adhabu itatolewa kwa kituo husika,” alisema Mbawala.
Kadhalika aliwashauri wanunuzi kuhakikisha wanapata stakabadhi ya malipo inayoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.
Alisema stakabadhi hiyo ya malipo itatumika kama kidhibiti cha mnunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo; au endapo atakuwa ameuziwa mafuta yenye kiwango cha ubora kisichofaa.
Mbawala alisema kutokana na mabadiliko hayo, jijini Dar es Salaam kuanzia leo, bei ya petroli ya rejareja kwa lita moja sasa itauzwa hadi Sh. 2,063; (dizeli-Sh. 2,016) na (mafuta ya taa-Sh. 1,976).
Kwa upande wa bei za jumla za mafuta, Mbawala alisema petroli itauzwa kwa Sh. 1,995.81 (dizeli-Sh. 1,948.50) na (mafuta ya taa-Sh. 1,908.53).
Arusha bei ya rejareja (petroli-Sh. 2,147); (dizeli-Sh. 2,100) na (mafuta ya taa-Sh. 2,060). Dodoma (petroli-Sh. 2,122); (dizeli-Sh. 2,075) na (mafuta ya taa-Sh. 2,035). Mbeya (petroli-Sh. 2,170); (dizeli-Sh. 2,123) na (mafuta ya taa-Sh. 2,083). Mwanza (petroli-Sh. 2,213); (dizeli-Sh. 2,166) na (mafuta ya taa-Sh. 2,126).
Kibaha (petroli-Sh. 2,068); (dizeli-Sh. 2021) na (mafuta ya taa-Sh. 1,981). Iringa (petroli-Sh. 2,127); (dizeli-Sh. 2,080) na (mafuta ya taa-Sh. 2,040). Bukoba (petroli-Sh. 2,278); (dizeli-Sh. 2,231) na (mafuta ya taa-Sh. 2,191).
Kigoma (petroli-Sh. 2,294); (dizeli-Sh. 2,247) na (mafuta ya taa-Sh. 2,207). Moshi (petroli-Sh. 2,137); (dizeli-Sh. 2,090) na (mafuta ya taa-Sh. 2,050).
Lindi (petroli-Sh. 2,122); (dizeli-Sh. 2,075) na (mafuta ya taa-Sh. 2,035). Babati (petroli-Sh. 2,185); (dizeli-Sh. 2,138) na (mafuta ya taa-Sh. 2,098). Musoma (petroli-Sh. 2,241); (dizeli-Sh. 2,194) na (mafuta ya taa-Sh. 2,154).
Morogoro (petroli-Sh. 2,088); (dizeli-Sh. 2,041) na (mafuta ya taa-Sh. 2,001). Mtwara (petroli-Sh. 2,136); (dizeli-Sh. 2,088) na (mafuta ya taa-Sh. 2,048). Sumbawanga (petroli-Sh. 2,236); (dizeli-Sh. 2,189) na (mafuta ya taa-Sh. 2,149).
Songea (petroli-Sh. 2,186); (dizeli-Sh. 2,139) na (mafuta ya taa-Sh. 2,099). Shinyanga (petroli-Sh. 2,192); (dizeli-Sh. 2,145) na (mafuta ya taa-Sh. 2,105). Singida (petroli-Sh. 2,154); (dizeli-Sh. 2,106) na (mafuta ya taa-Sh. 2,067). Tabora (petroli-Sh. 2,217); dizeli-Sh. 2,170) na mafuta ya taa-Sh. 2,130). Tanga (petroli-Sh. 2,109); (dizeli-Sh. 2,062) na (mafuta ya taa-Sh. 2,022).