Siku chache baada ya msanii na prodyuza wa muziki wa kizazi kipya, Raheem Rummy Nanji ‘Bob Junior’ (pichani kushoto mwenye nywele za kusokota) kupokea tuzo kutoka kwa aliyekuwa hasimu wake Naseeb Abdul ‘Diamond’ (pichani kushoto mwenye miwani) imebainika kuwa walishamaliza bifu lao lililodumu kwa muda mrefu, Fleva Mchanganyiko inakuhabarisha.

Akifichua kilichokuwa nyuma ya pazia, Bob Junior alisema kwamba, Diamond alimpigia simu na kumuomba radhi kabla ya kumwalika kwenye ‘bethidei’ yake iliyofanyika Oktoba 2, mwaka huu katika Klabu Maisha jijini Dar.
“Diamond alinipigia simu na kutaka tuyamalize na nishiriki katika sherehe yake ya kuzaliwa, nikatafuta ushauri kwa vijana wakanitaka nimpotezee lakini wazee pamoja na mama yangu mzazi wakaniambia nimsikilize na kushirikiana naye, nami nikaukubali ushauri huo wa wazee,” alisema Bob Junior.

Prodyuza huyo ambaye alidaiwa kugombana na Diamond kwa kudaiwa kumkatalia kumfanyia kazi yake, alisema kuwa sasa tofauti zao zimekwisha na wanajiandaa kufanya kazi pamoja.

Diamond alisherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa kuwazawadia tuzo watu mbalimbali waliofanikisha uwepo wake katika muziki na kumvisha pete ya uchumba mpenzi wake anayetamba katika filamu, Wema Sepetu.