Na Musa Mateja
IMEBAINIKA kuwa katika mikikimikiki ya kimapenzi, kumbe Wema Isaac Sepetu (pichani) ana pete tatu kwa wanaume tofauti, moja ya ndoa na mbili za uchumba, Amani linafunguka.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti hili, Wema aliyevishwa pete ya uchumba na mwanamuziki Naseeb Abdul Juma ‘Diamond’ hivi karibuni, Februari, 2009 alivishwa pete ya ndoa na aliyekuwa mpenzi wake wakati huo, Mjasiriamali Jumbe Yusuf Jumbe.

ASAKWA AREJESHE PETE
Haukupita muda mrefu, Wema anayeshikilia taji la umalkia wa urembo Bongo 2006/07,
alikorofishana na Jumbe kwa maneno ya shombo kwenye vyombo vya habari ambapo jamaa huyo amekuwa akimsaka ili amrudishie pete yake.

Baada ya ‘kukinukisha’ kwa Jumbe, Wema alitua mzima mzima kwa mwanamuziki ‘the big name’ wa Bendi ya The African Stars International ‘Twanga Pepeta’, Charles Gabriel Mbwana ‘Chalz Baba’.

CHALZ BABA ATOA YA MOYONI
Mwishoni mwa wiki iliyopita Chalz Baba aliibuka na kutoa ya moyoni mwake mbele ya paparazi wetu kuwa, mwaka 2010 kabla ya Wema kutimkia Marekani, naye alimvisha mrembo huyo pete ya uchumba kwa ahadi kuwa akirejea Bongo watafunga ndoa.

Chalz Baba alifunguka kuwa, Wema alimtenda vibaya kwani hata kabla ya kurejea Bongo ili kutimiza ahadi yao ya kufunga pingu za maisha, mambo yaliharibika, wakatemana kwa kashfa kama ilivyokuwa kwa Jumbe.

“Ukweli ni kwamba hata mimi nilimvisha pete ya uchumba, sema tu sikufanya ‘ofisho’ sana. Ilikuwa ni ‘promisi’ kati yangu na yeye. Tulipoachana hakunirudishia ‘so’ atakuwa nayo,” alisema Chalz Baba.

ASHAURIWA KUMUOMBA MUNGU
Chalz Baba anasema: “Namjua Wema vizuri, anatakiwa amuombe sana Mungu amuwezeshe kudumu na Diamond kwani kwa uwezo wake nina uhakika asilimia 99 hatafikia lengo la kufunga ndoa.”

KANUMBA VIPI?
Kabla ya kuingia mikononi mwa Jumbe, Wema alikuwa laazizi wa Steven Charles Kanumba hivyo alipotakiwa kuzungumzia tukio la mrembo huyo kuvishwa pete ya ‘in’gejimenti’ na Diamond alicheka kidogo ‘teh…teh…teh’ kisha akasema: “No comment.”

Habari kwa Hisani ya Global Publisher.