SERIKALI imesema imechoshwa na timu ya taifa kuboronga na ikaeleza kuwa tatizo halichangiwi na makocha wanaokuja isipokuwa kasoro ipo kwenye maandalizi.

“Tutamlaani kila kocha ajaye, tutasema fukuza huyu, kumbe tatizo si kocha bali sisi hatujafanya maandalizi,” alisema Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi.

Dk. Nchimbi alikuwa akijibu swali la mkazi wa Butiama, Eliud Elmon katika mdahalo ulioandaliwa kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kufahamu undani wa wizara hiyo ambayo inaadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara kijjini Butiama, mkoani Mara.

Elmon alitaka kufahamu mpango wa Serikali uliopo kuhakikisha timu ya taifa inasonga mbele kutokana na kuvurunda katika mashindano mbalimbali.

Dk. Nchimbi alisema Serikali imefanikiwa kuunda vikundi na taasisi za michezo huku changamoto ikiwa ni kwenda kwenye ubora.

“Serikali imechoshwa na timu kushindwa. Nikiwa Uwanja wa Taifa sina uvumilivu. Nikizidiwa, huwa natoka najifanya naongea na simu. Sitaki kuona tunafungwa,” alisema Nchimbi.

Alieleza namna anavyoguswa na timu ya taifa kufungwa na kusema mwanzoni kabla ya kuwa waziri mwenye dhamana ya michezo, alikuwa hataki kwenda uwanjani na kushuhudia ikifungwa.

Hata hivyo alisema kwa kuwa sasa ana dhamana hiyo, hulazimika kwenda. “Nilikuwa siendi lakini sasa nalazimika kwenda. Naishi maisha ya tabu…,” alisema.

Akizungumzia suala zima la maandalizi ya timu, Waziri Nchimbi aliendelea kusisitiza umuhimu wa vyama vya michezo kuhakikisha vinasaka vipaji na kuwatumia watoto.



Alisema ameshaagiza vyama vya michezo vya kitaifa vizingatie hilo. Alisema wakati nchi zilizoendelea huwashirikisha watoto wakiwa na umri wa kuanzia miaka 10, nchini vilabu vinavizia wenye umri kuanzia miaka 17 jambo ambalo ni tatizo.

“Wenzetu wanaanzia miaka 10 Sisi tunaviziana miaka 17… akipigwa chenga mbili anatenguka nyonga,” alisema Dk. Nchimbi na kusisitiza kwamba chini ya mkakati wa miaka mitano wa kukuza michezo, ushirikishaji watoto hauna budi kutekelezwa.

Pamoja na kuviagiza vyama vya michezo vitekeleze hilo, Dk. Nchimbi alisema pawepo bajeti ya kimichezo baada ya kuainisha mikakati ya kufanya ili kukuza sekta hiyo.

Vyama vya michezo vimetajwa kuwa na jukumu la kuandaa mpango wa taifa ili ufanyiwe kazi. Hata hivyo, alisema mpango husika hauwezi kuwa wa siku moja.

“Hauwezi kuwa na mpango wa siku moja, ukamilike leo mwakani tuingie kombe la dunia,” alisema. Wakati huo huo, katika mdahalo huo, suala la vijana kuiga utamaduni wa nje ikiwemo wasanii wanaocheza nusu uchi, lilihojiwa.

“Utamaduni wa Mtanzania, tulikuwa hatuchezi uchi. Hamuoni hii inaleta aibu kuona sehemu zisizotakiwa kuonekana, zinaonekana wakati wa kucheza,” alihoji Blasius Chuma.

Akijibu hilo, Waziri alisema kila mtu binafsi anapaswa aone thamani ya utu wake. Alisema heshima ya mtu mmoja mmoja inagusa heshima ya mtu mwingine.

“Kila mtu mahala alipo auwakilishe Utanzania na kufanya mambo ambayo yataifanya nchi ionekane imestaarabika,” alisema.