SERIKALI imesema hadi kufikia Desemba mwaka huu asilimia 75 ya wakazi wa Dar es Salaam watapata maji safi na salama chini ya Mpango wa Sekta ya Maji nchini (WSDP).

Aidha, imesema tangu kuanza kwa mpango huo, fedha zilizotengwa na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo zimeongezeka kutoka dola za Marekani milioni 951 hadi dola bilioni 1.2 hadi Juni mwaka huu.

Naibu Waziri wa Wizara ya Maji, Gerson Lwenge alisema katika makao makuu ya wilaya pamoja na miji midogo huduma nchini imefikiwa kwa asilimia 53 na kwa Jiji la Dar es Salaam kwa sasa ni asilimia 55.

Lwenge aliyasema hayo jana Dar es Salaam katika mkutano wa sita wa wadau wa sekta ya maji uliokuwa ukijadili mpango wa miaka mitano wa utoaji wa huduma ya maji nchini.

“Pamoja na mafanikio hayo, zipo changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuchelewa kwa mipango ya maendeleo ya mwaka 2010/11 na 2011/ 12 kutokana na kutokuwepo kwa fedha zilizolipwa kwa wafadhili tangu Machi 2010,” alisema.

Hata hivyo, alisema kuongezeka kwa fedha kutaisaidia Serikali kutekeleza mipango yake katika sekta ya maji na kuwezesha kufikiwa kwa malengo ya Mkakati wa Taifa wa Kupunguza Umaskini (MKUKUTA).