MFANYABIASHARA Harden Hermany (39) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala akikabiliwa na mashitaka ya wizi wa tiketi ya ndege ya Precision.
Hermany ambaye alikana mashitaka na kurudishwa rumande, alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda.
Wakili wa Serikali Honorina Munishi alidai kuwa, Oktoba 13 mwaka huu saa 12 jioni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Hermany alikamatwa na Inspekta Dennis Moyo akiwa na tiketi yenye namba 0312410713277.
Ilidaiwa kuwa tiketi hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya safari ya kutoka Dar es Salaam kwenda Johannesburg, Afrika Kusini na kurudi kwa ndege namba PW 200.
Inadaiwa siku hiyo Hemany alitumia tiketi hiyo kujipatia dola za Marekani 545, mali ya kampuni ya shirika hilo.
Hermany anadaiwa pia kutoa Sh 900,000 kwa mfanyakazi wa shirika hilo, Jerry Ngieve ili asiseme kitendo alichokifanya jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Alikana shitaka na upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika. Kesi hiyo itatajwa Oktoba 31 mwaka huu.
0 Comments