Mbunge wa Kyela mkoani Mbeya, Dk. Harrison Mwakyembe, ameanza kupewa dawa baada ya madaktari bingwa wa Hospitali ya Indraprasta Apollo iliyopo nchini India alikolazwa kumaliza kazi ya kumchunguza afya yake kwa kumchukua vipimo na kubaini kinachomsumbua.
Katibu wa mbunge huyo, Salum Nkambi, akizungumza kwa simu, alisema Dk.Mwakyembe ameanza kupewa dawa baada ya madaktari kumaliza hatua ya kwanza ya kumchukua vipimo ambapo wamebaini ugonjwa unaomsumbua.
Nkambi ambaye hata hivyo hakuweka wazi majibu yaliyotolewa na madaktari kuhusu ugongwa unaomsumbua Dk. Mwakyembe kwa maelezo kuwa kazi hiyo itafanywa na madaktari kuelezea umma kinachomsumbua.
Alisema hata hivyo, hali ya Dk. Mwakyembe imeendelea kuwa nzuri tangu alipoanza kupatiwa dawa hizo.
Hata hivyo habari ambazo  tumezipata ni kwamba serikali imemtuma mtaalam mmoja kwenda India ambaye kufuatilia majibu yaliyotolewa na madaktari wa hospitali hiyo.

Dk. Mwakyembe alipelekwe India mapema wiki iliyopita kwa ajili ya matibabu. Kabla ya kuondoka nchini baadhi ya vyombo vya habari vilimkukuu mke wa Dk. Mwakyembe, Linah, yalisema Dk. Mwakyembe anasumbuliwa na ugonjwa wa ngozi unaojulikana kitaalamu kama Exfoliative Dermatitis.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni, alisema hali ya Dk Mwakyembe ni nzuri na kwamba anaendelea na matibu na kuwa anawasiliana naye kila siku.
Kuhusu madai kuwa Dk. Mwakyembe alipewa sumu, alisema hawezi kuzungumzia taarifa hizo kwa kuwa hazina ukweli.
CHANZO: NIPASHE