Kwa mujibu wa tangazo lilitolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha katika baadhi ya vyombo vya habari jana, wastaafu wote ambao malipo yao ya pensheni yanalipwa na Hazina kila baada ya miezi sita, sasa watakuwa wakilipwa kila baada ya miezi mitatu kuanzia Januari, 2012.
Tangazo hilo la serikali limefafanua kuwa mabadiliko hayo yametokana na maombi ya wastaafu kupitia vyama vyao kutoka katika baadhi ya mikoa, wastaafu binafsi na baadhi ya maombi ya wstaafu binafsi kupitia kwa wabunge.
"Kwa ajili hiyo, malipo ya pensheni yatakayolipwa mwezi Januari, 2012 yatakuwa ya miezi mitatu ya Januari, 2012 hadi Machi, 2012 na malipo ya miezi mitatu ya Aprili, 2012, hadi Juni, 2012, yatalipwa mwezi Aprili, 2012. Utaratibu wa miezi mitatu mitatu ndio utakaoendelea kutumika," lilifafanua tangazo hilo.
Chini ya utaratibu wa sasa, wastaafu wamekuwa wakilipwa pesheni yao kila baada ya miezi sita sita ambapo hulipwa Januari na Julai ya kila mwaka.
Kima cha chini kwa wastaafu hao ni Sh. 50,000, kiasi ambacho kwa muda mrefu kimekuwa kikipigiwa kelele na wastaafu wenyewe na wawakilishi wao bungeni kwa maelezo kwamba hakikidhi mahitaji hasa kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha.
Wengi wa wastaafu na wabunge wamekuwa wakiiomba na kuishauri serikali iangalie upya kiwango hicho ili angalau kiendane na hali halisi ya kupanda kwa maisha.
Aidha, wamekuwa wakishauri kuwa ni vema viwango vya pensheni vya wastaafu viwe vinabadilika kulingana na mabadiliko ya mishahara kwa cheo alichostaafia.
0 Comments