Maafisa wa Ufaransa wametangaza kuwa mama raia wa kifaransa aliyetekwa nyara kutoka Kenya na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Kisomali mapema mwezi huu amefariki.


Maafisa wa kibalozi wanasema walifahamishwa kifo cha Marie Dedieu na watu ambao wamekuwa wakijaribu kuzungumza na watekaji nyara ili wamuachie huru mama huyo.
Wamesema kuwa hawajui alikufa lini na nini kilichosababisha kifo chake, ingawa inakumbukwa kuwa afya yake ilikuwa dhaifu na kuwa hakuruhusiwa kutumia dawa, tukio kama hili lilitarajiwa.


Bi. Dedieu mwenye umri wa miaka 66 ni mmoja wa wageni kutoka mataifa ya magharibi waliotekwa kutoka Kenya mwezi October.


Mwezi September raia kutoka Uingereza David Tebbutt aliuawa na mke wake Judith kutekwa katika hoteli moja ya kifahari huko Kiwayu pwani ya Kenya.



Na mwezi jana wanawake wawili raia wa Uhispania wafanyakazi wa misaada walitekwa kutoka kambi ya wakimbizi ya Dadaab karibu na mpaka wa Kenya na Somalia.

Wanawake wote watatu waliotekwa bado hawajulikani walipo.

Bi.Dedieu ambaye alitumia kiti cha magurudumu na dawa kila mara kutokana na matatizo ya moyo na vile vile saratani, alikuwa akiishi Kenya tangu miaka ya 90.

Alitekwa nyara kutoka nyumbani kwake katika kisiwa kidogo cha Manda katika eneo la Lamu tarehe moja mwezi October na watu waliokuwa na silaha.


Maafisa wamethibitisha alisafirishwa kwa boti hadi Somalia na kuwa waliomteka nyara hawakuchukuwa kiti chake cha magurudumu ama dawa zake wakati wakimteka.