CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kwamba ushindi wake katika ubunge wa Igunga na kata 17 kata ya 22 zilizofanya Uchaguzi Mdogo nchini mwishoni mwa wiki ni uthibitisho kwamba wananchi wameyakubali mageuzi ndani ya chama hicho.

Chama hicho kimekilaumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kusababisha watu wachache wajitokeze kupiga kura Igunga, kwa kujenga hofu iliyotokana na matukio ya vurugu za chama hicho.

Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

“Ushindi wetu wa ubunge katika Jimbo la Igunga na udiwani katika kata 17 kati ya 22, ni uthibitisho kwamba mageuzi tunayofanya ndani ya chama yanakubalika kwa wananchi,” alisema Nape na kuongeza: 

“Maana wapo waliokuwa wanadai kwamba mageuzi haya yatakiua Chama, lakini imedhihirika kwamba ni mageuzi yanayokisaidia chama na kukipa uhai zaidi.”

CCM ilishinda ubunge wa Igunga Jumapili iliyopita kwa mgombea wake, Dalaly Kafumu kuibuka mshindi kwa kura 26,484 na kumshinda mpinzani wake wa karibu, Joseph Kashindye wa Chadema aliyepata kura 23,260.

Kiti hicho kilikuwa wazi kutokana na kujiuzulu kwa Rostam Aziz, Julai 14, mwaka huu baada ya kuwa mwakilishi wa jimbo hilo la Mkoa wa Tabora kwa takriban miaka 17.

Akizungumzia suala la wapigakura wachache katika uchaguzi huo, Nape aliitupia lawama Chadema kwa kusababisha hali hiyo.Wananchi 53,672 walijitokeza kupiga kura kati ya watu 171,019 walioandikishwa katika daftari la wapigakura.



“Chadema wanapaswa kulaumiwa kwa hili, matukio ya kumwagiwa tindikali kwa kijana wa CCM, kudhalilishwa kwa Mkuu wa Wilaya, kuingizwa kwa vijana zaidi ya 800 kutoka nje ya Igunga, yaliwatisha watu wengi hasa kinamama na wenye umri mkubwa.

“Hawa wasingeweza kujitokeza kupiga kura kwa sababu tayari mazingira yalionesha kwamba kutakuwa na fujo hivyo wakaogopa kwenda kupiga kura.”

Aidha, CCM imewashukuru kwa dhati wananchi kwa uamuzi wao wa kuendelea kukiamini na kukipa dhamana kwa kura nyingi.

“Imani hii ni deni kwetu na tunawahakikishia tutalipa kwa kuwatumikia kwa uaminifu,” alisema Nape na kuwataka wanachama wake waliochaguliwa kuhakikisha wanasimamia Ilani ya Uchaguzi ya CCM itekelezwe kikamilifu kwa sababu ndiyo tuliitumia kuwanadi.

Mbali ya kuvipongeza vyombo vyote vya habari kwa kufanya kazi kubwa na nzuri ya kuwapa habari wananchi kuhusu mwenendo mzima wa kampeni hizo na Uchaguzi Mdogo wa Igunga, lakini Nape alikuwa na angalizo.

“Tunaamini mwisho wa chaguzi hizi ni wakati mzuri kwa vyombo vyote vya habari nchini kukaa chini na kutathimini jinsi walivyotimiza wajibu wao kwa umma wakati wa kuripoti matukio mbalimbali,” alisema Nape.

Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi, alisema kutokana na ushindi huo, kimeandaa ratiba fupi ya awali ya kuwashukuru wananchi wa Igunga na maeneo mengine yaliyofanya uchaguzi kwa kuichagua CCM.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, jana na leo kutakuwa na sherehe mkoani Singida, kesho ni zamu ya Dodoma, Ijumaa ni Pwani na siku inayofuata ni Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema amesema tofauti zilizotokea katika uchaguzi wa Igunga zimesababishwa na tofauti za itikadi ingawaje uchaguzi ulifanyika kwa hali ya utulivu na amani.

IGP Mwema aliwaambia waandishi wa habari jana Dar es Salaam kuwa uvumilivu na utulivu ni ishara ya ukomavu wa demokrasia.

Alisema uvumilivu uliooneshwa katika jimbo hilo ni ishara ya kukomaa kwa demokrasia na kwamba wananchi waendelee kufuata kanuni na taratibu.

Kadhalika alilipongeza Jeshi la Polisi kwa ushirikiano walioonesha katika mchakato wote na kuwataka wananchi kufuata sheria bila kushurutishwa ili kuendelea kuikomaza demokrasia kwa kuzingatia haki na wajibu.

Kuhusu haki bila shuruti, alisema anahamasisha wananchi haswa vijana kutoa taarifa katika matukio mbalimbali yatakayoashiria uvunjifu wa amani.

Mjini Igunga, huduma za kijamii zimerejea tena jana baada ya siku zima ya juzi kusimama kwa huduma zote kuanzia maduka masoko na migahawa kutokana na hofu iliyotanda mjini humo ya uwezekano wa fujo baada ya matokeo ya uchaguzi.

Mkazi wa mji huo, Sarah Maganga alisema juzi watu wengi walikuwa wanaihofia hali ilivyokuwa kwani kabla ya matokeo kutangazwa, hali ilikuwa si shwari na kwamba watu hawakutoka hata kushangilia ushindi wa CCM kwa hofu ya kutokea fujo.

“Watu wa Igunga hasa wenyeji na wasiopenda fujo kabisa kutoka na hali ilivyokuwa wasingeweza kufungua maduka yao na soko kufunguliwa na kwa upande wa sokoni, watu walitoa hata bidhaa zao kwa kuhofia soko kuchomwa moto,” alisema Sarah.