KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imesema haijaridhishwa na namna Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inavyosimamia ukaguzi hasa katika masomo ya Hisabati na Sayansi.

Pia Kamati hiyo imetoa agizo kwa Wizara hiyo kutafuta njia itakayowezesha kuondoa nguvu aliyonayo Waziri wa Elimu ya kubadili mitaala anavyoona, jambo ambalo linachangia kuathiri mfumo mzima wa elimu.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, John Cheyo wakati wa mjadala wa Kamati hiyo juu ya ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inayohusu kufeli kwa wanafunzi katika masomo ya Hisabati na Sayansi na namna ukaguzi unavyoweza kusaidia kumaliza tatizo hilo.

“Majibu yenu yanaonesha kuwa idadi ya wakaguzi wa Hisabati na Sayansi tangu mwaka 2008 hadi sasa ni 58 kati ya shule zaidi ya 4,000 hii ni hatari, inaonesha kabisa eneo hili kwa muda mrefu halijapewa kipaumbele,” alisema Cheyo ambaye ni Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP).

Alisema wakati hali ya ukaguzi ikiwa hivyo, ripoti ya CAG inaonesha kuwa katika matokeo ya kidato cha nne tangu mwaka 2004, 2005 na 2006, ufaulu wa masomo ya Hisabati ulishuka kwa asilimia 70, 77 na 76 na masomo ya Fizikia, Kemia na baolojia kwa asilimia 45, 35 na 43.

Aidha, alisema CAG pia alikagua eneo la ukaguzi shuleni na kubaini kuwa matokeo ya ukaguzi hayana mpango mkakati kuhusu matokeo hayo mabaya ya wanafunzi, hayaoneshi vipaumbele vya namna ya kusaidia wanafunzi wanaofanya vibaya na ripoti hizo za ukaguzi hazioneshi njia za kutatua tatizo.

“Tunagusia eneo la ukaguzi kwa kuwa unatupa mwelekeo wa kuzuia watoto wetu wasifeli masomo yao, hatusemi kuwa ukaguzi ndio chanzo, lakini tukubali kuwa ndio msingi kwani usipojengwa kazi ya ualimu haifanyiki kiufanisi,” alisema Cheyo.



Pia Cheyo aliitaka Wizara pia kuangalia eneo la kubadilishwa mara kwa mara kwa mitaala ambako kunatokana na nguvu aliyonayo Waziri jambo ambalo pia linachangia wanafunzi kufeli mitihani yao na aliitaka Wizara hiyo kuandaa muswada wa sheria kuhusu suala hilo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Khamis Dihenga, alisema Wizara hiyo iliipokea ripoti ya CAG na kuanza kuifanyia kazi mara moja na katika eneo la ukaguzi na waliamua kushirikisha Idara ya Elimu ya Msingi na Sekondari ili kuwa na ufanisi.

Alikiri kuwa tatizo la uhaba wa wakaguzi ni kubwa ambapo kwa sasa kuna wakaguzi wa shule ya msingi 1,052 wakati wanaohitajika ni 1,450, sekondari na vyuo waliopo ni 138 wanaohitajika 252 na wakaguzi wa masomo ya Hisabati na Sayansi waliopo ni 58.