Kenya inasema jeshi lake liko tayari kuvuka mpaka na kuingia Somalia, kuwaandama watekaji nyara wanaowateka wageni.
Waziri wa Usalama wa Nchi, George Saitoti, alisema jeshi litawasaka wafuasi wa kikundi cha waislamu wenye siasa kali, al Shabaab, kokote waliko.

Alisema kuwa mpaka wa Kenya na Somalia umefungwa.

Na alihusisha utekaji nyara na mmiminiko wa watu kutoka Somalia, wanaokimbia ukame mkali, na ombi la kimataifa kuwa Kenya iwape hifadhi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Saitoti alisema:

"Sasa tumefunga mpaka na wala hatuombi msamaha kwa kufanya hivo.

Mtakumbuka kuwa wakimbizi wengi walipokuwa wanaingia kutoka Somalia, kwa sababu ya ukame huko, tulikubali kuwapokea, kutimiza wajibu wetu wa kimataifa.

Lakini piya tulionya ulimwengu kwamba ingawa Kenya ilikuwa tayari kuwapokea hawa watu, lakini kulikuwa na hatari kuwa siyo wote kutoka Somalia walikuwa kweli wakimbizi; na kwamba pengine walikuwamo wafuasi au wanachama wa Al Shabaab.


Sisemi kuwa hatujawakagua.

Tulijitahidi kuwakagua.

Na sasa, hii kambi ya wakimbizi ambayo ndio kubwa kabisa duniani, tutafanya ukaguzi mwengine wa watu waliomo humo"

Hapo awali shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi, UNHCR, lilisimamisha shughuli zisokuwa muhimu katika kambi hiyo ya Dadaab, ambako wasaidizi wawili kutoka Uspania walitekwa nyara siku ya Alkhamisi.

Al-Shabaab inakanusha kuwa ilihusika.

Waziri wa Ulinzi wa Kenya, Yusuf Haji, alisema wanawake hao wawili hawakufuatana na mlinzi, na pengine hawakutekwa nyara.

Waziri Haji alisema:

"Hawa mabibi walikuwa ndani ya gari binafsi, na hawakuwa na mlinzi.

Habari tulizonazo ni kuwa gari lao limenasa pahala.

Wameliacha na sasa wanatembea kwa miguu.

Kwa hivo ikiwa wamejificha chini ya mti itakuwa shida kuwapata kwa urahisi, lakini tunatumai wakionekana, wataokolewa."