WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige amemtema cheche na kuyakataa majibu ya Kaimu Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini, Paul Sarakikya aliyetakiwa kutoa ufafanuzi juu ya mwekezaji katika kijiji cha Mitimirefu, wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro anayedaiwa kutorosha wanyama nje ya nchi kinyume cha sheria.
Pamoja na kuyakataa majibu hayo, amemtaka Kaimu Mkurugenzi huyo kutoondoka kijijini hapo ili afanye uchunguzi na kukabidhi majibu kufikia Jumanne ijayo.
Hayo yalitokea wakati wa mkutano wa hadhara kijijini hapo ambako wakazi wa kijiji hicho walimtuhumu mwekezaji huyo, kampuni ya Ndarakwai Camp mbele ya Waziri Maige, kuwa amekuwa akitorosha wanyama kwenda nje ya nchi, kinyume cha sheria.
Walidai kuwa, mwekezaji huyo aliwekeza kjijini hapo kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo kwenye shamba la Ndarakwai, lakini alibadilisha shughuli zake na kuanza utalii wa picha kwa kuweka vivutio vya wanyama bila ya kuwa na kibali cha Wizara ya Maliasili na Utalii.
Walisema kuwa kibaya zaidi mwekezaji huyo amekuwa akisafirisha wanyama kwenda nje ya nchi kinyume cha sheria, na kwamba katika shamba lake kulikuwa na wanyama aina ya pofu wanne, nyumbu mmoja na pundamilia wawili, lakini baadaye wanyama hao walitoweka katika mazingira ya kutatanisha, na kwamba huenda walisafirishwa na mwekezaji huyo kwenda nje ya nchi.
Baada ya wananchi hao kutoa madai hayo, ndipo Waziri Maige alimtaka Kaimu Mkurugenzi huyo kutoa majibu kwa wananchi hao.
“Mkurugenzi sasa nakutaka utoe majibu kuhusu maswali hayo ya wananchi yanayohusu idara yako ya wanyamapori, hasa suala hilo la kudaiwa kuwa mwekezaji huyo anatorosha wanyama wetu,” aliagiza Waziri Maige.
Mara baada ya kusimama, Kaimu Mkurugenzi huyo alijibu: “Kuhusu suala kwamba kulikuwa na wanyama katika shamba hilo na sasa hivi hamuwaoni, hilo mimi siwezi kujua maana wanyama nao wana maisha yao…hivyo wanaweza kuugua na kufa na hivyo mkakosa kuwaona katika eneo hilo.”
Akaongeza kusema: “Kuhusu suala kwamba aliwekeza katika eneo hili kwa shughuli za kilimo na sasa amebadilisha matumizi ya ardhi na kuanza utalii wa picha…hilo suala la ardhi mimi siwezi kulizungumzia hapa.”
Baada ya majibu hayo, Waziri Maige alisimama na kusema kwamba, kamwe haridhiki na majibu hayo ambayo aliyaita kuwa ni mepesi mno na pia ni ya ubabaishaji mtupu, kuhusu jambo hilo nyeti.
Alisema alitegemea Kaimu Mkurugenzi huyo angetoa majibu ya kina ikiwa ni pamoja na kukerwa na kitendo hicho cha utoroshaji wa wanyama nje ya nchi kama ni kweli limekuwa likifanyika.
“Mimi nilitegemea nimalize ziara yangu vizuri, lakini sasa huyu mkurugenzi amenitibua sana, unatoa majibu mepesi mepesi kiasi hicho, wakati hawa wananchi wanatupatia taarifa kwamba huyo mwekezaji amekuwa akitorosha wanyama kwenda nje ya nchi, halafu wewe unajibu majibu mepesi kiasi hiki.
“Nakuagiza kwamba ubaki huku ili ukague shamba hilo kama kuna wanyama na kama mwekezaji huyo amekuwa akitorosha wanyama kama inavyodaiwa na hawa wananchi na wananchi hawa hawawezi kusema maneno ya uongo…nilitegemea utoe majibu mazuri…sasa ninataka ufanye uchunguzi haraka na taarifa ya uchunguzi huo uniletee tarehe moja mwezi ujao (Jumanne ijayo),” alisema Waziri Maige kwa hasira.
Sarakikya amejikuta akipatwa na mtihani huo ikiwa ni miezi miwili na nusu tangu akaimu nafasi hiyo, baada ya aliyekuwa anashika nafasi hiyo, Obeid Mbangwa kusimamishwa na serikali ili kupisha uchunguzi wa usafirishaji wa wanyamapori hai wenye thamani ya Sh milioni 116 na ndege 16 uliofanyika Novemba 24, mwaka jana kwenda nje ya nchi kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Uamuzi wa kumsimamisha Mbangwa na maofisa wengine wawili wa idara hiyo ulitangazwa Agosti 17 mwaka huu na Waziri Maige wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Wizara yake bungeni mjini Dodoma.
Mara baada ya Maige kutoa kauli hiyo, Mbangwa ambaye alikuwa mmoja wa maofisa wa wizara waliokuwa kwenye ukumbi wa Bunge, alitoka nje na alionekana akikimbia kutoka nje ya eneo la bunge.
Mbangwa alikuwa mkurugenzi mpya wa idara hiyo akichukua nafasi ya mtangulizi wake Erasmus Tarimo, aliyestaafu kwa mujibu wa sheria. Wakati Tarimo akiwa Mkurugenzi, Mbangwa alikuwa Mkurugenzi Msaidizi (Matumizi Endelevu).
0 Comments