Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akimpa pole Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhumbili kabla ya kupelekwa India. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

VIONGOZI zaidi wamelazwa katika hospitali za ndani na nje ya nchi kwa uchunguzi wa afya na wengine wakiugua magonjwa mbalimbali.
Taarifa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, zimeeleza kuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, aliyelazwa hospitalini hapo, amekutwa na vijidudu 150 vya malaria na anaendelea vizuri chini ya uangalizi maalumu wa madaktari.

Jana kulikuwa na uvumi uliosambaa kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu za mkononi (sms)kuwa Zitto amefariki dunia.

Wakati Zitto akipata matibabu, Mbunge wa Viti Maalumu, Clara Mwituka (CUF), naye alifikishwa hospitalini hapo juzi na kupokewa chini ya Idara ya Wagonjwa wa Dharura kutokana na kusumbuliwa na vidonda vya tumbo.

Msemaji wa hospitali hiyo, Jezza Waziri, alisema jana kuwa wataalamu wanaomtibu Zitto walibaini kwamba anasumbuliwa na malaria na kukutwa na vijidudu hivyo mwilini.



“Tofauti na jana (juzi) alipofikishwa hapa, leo (jana) hali yake inaendelea vizuri na yuko chini ya uangalizi maalumu akiendelea na matibabu,” alisema Waziri.

Kuhusu Mwituka, alisema alifikishwa hospitalini hapo akisumbuliwa na vidonda vya tumbo, na kwamba kama ilivyo kwa Zitto, pia anaendelea na matibabu chini ya uangalizi wa madaktari.

“Ataendelea kuangaliwa katika kitengo hicho kwa saa 24, na baada ya hapo hali yake ikionekana kuendelea vizuri atapelekwa katika wodi za kawaida kuendelea na matibabu,” aliongeza Waziri.

Gazeti hili liliwashuhudia wabunge kadhaa wakifika hospitalini hapo jana kuwajulia hali Zitto na Mwituka.

Wakati kukiwa na madai kwamba Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe aliyelazwa India amelishwa sumu, uongozi wa Polisi nchini umesema utachukua hatua za kisheria endapo watapata taarifa sahihi kwamba kiongozi huyo amelishwa sumu.

Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, Samson Kassala, alisema hayo jana wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari likiwamo la kutaka kufahamu ni hatua gani za kisheria zilizochukuliwa kutokana na madai kwamba Dk. Mwakyembe amelishwa sumu.

“Tunachofanya sasa tunasubiri uchunguzi wa daktari, tukishapewa taarifa tutazifanyia kazi, sisi tuko tayari wakati wote kupokea taarifa na aliyenazo anakaribishwa,” alisema Naibu Kamishna wa Polisi Kassala.

Hata hivyo, alifafanua kuwa ugonjwa wa mtu ni siri yake na daktari, na ndiyo maana wanasubiri hizo taarifa ndipo zifanyiwe kazi.

Viongozi wengine waliolazwa kwa matibabu ni pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami ambaye alipelekwa India Jumanne kwa uchunguzi wa afya yake.

Mwingine ni Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya, ambaye amelazwa nchini humo kwa miezi kadhaa sasa, baada ya kufanyiwa upasuaji wa mgongo.