Na Waandishi wetu (kutoka michuzi)



Kikundi cha kigaidi cha Al-Shaabab kimezua hofu kuelekea kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara baina ya Simba na Yanga kesho baada ya Jeshi la Polisi nchini kutoa taarifa ya kuzuia mikusanyiko kwa kuwa wana taarifa kwamba kikundi hicho kina mpango wa kufanya mashambulizi jijini Dar es Salaam.



Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamezuia maandamano yaliyokuwa yafanyike kesho ya Mtandao wa Wanaharakati ya kupinga Serikali kuilipa kampuni ya umeme ya Dowans kwa kuwa Jeshi la Polisi nchini limepata taarifa kuwa kikundi hicho cha kigaidi kinapanga kufanya mashambulizi kwenye mikusanyiko ya watu jijini Dar es Salaam.



"Hatuwezi kuruhusu maandamano ya aina yoyote wala mikusanyiko mikubwa kwa njia ya mikutano ya hadhara hivyo maandamano yaliyokusudiwa na taasisi hizo yanasitishwa kwa sababu za kiusalama nilizozitaja," alisema Kova.



Hata hivyo, Kamanda Kova aliwataka mashabiki kufika kwa wingi katika mechi ya Simba na Yanga kushangilia timu zao kwa sababu uwanjani hapo kutakuwa na ulinzi wa uhakika na hata hivyo "Al Shabaab wanapenda kwenye mikusanyiko ya wanaharakati."



Kova alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, wamepanga mkakati madhubuti kuhakikisha kwamba mchezo huo unafanyika kwa amani na utulivu.



Kova alisema kiwango cha usalama na utulivu kilichokusudiwa kitamwezesha shabiki au mpenzi wa soka kwenda uwanjani na kuondoka kwa usalama, yeye pamoja na familia yake.



Alisema Jeshi la Polisi limechukua hatua madhubuti za kiulinzi na kiusalama, ambazo ni pamoja na kutoruhusiwa mtu yeyeyote kuingia na kilevi chochote uwanjani au kunywa kinywaji chochote chenye kilevi.



Alisema watu hawaruhusiwi kubeba silaha ya aina yeyote uwanjani kama vile kisu, panga na kadhalika na kwamba mashabiki hawaruhusiwi kuhama au kuvamia majukwaa ambayo ni tofauti na gharama za tiketi zao.



Alisema Jeshi la Polisi litaweka kamera maalum za video ili kuweka kumbukumbu na kubaini matukio yote yatakayojitokeza uwanjani kabla na baada ya mchezo huo na pia utupaji wa chupa zenye kimiminika cha aina yeyote hauruhusiwi na haivumiliki na hatua dhidi ya vitendo hivyo zitachukuliwa.



Vilevile alisema wale wote watakaobainika na makosa ya uhalifu, majina yao yatatangazwa pamoja na picha zao kuonyeshwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa lengo la kukomesha tabia mbaya za kihuni.



Alisema shabiki yeyote atakavamia "dimbani" wakati wa mpira ukichezwa kwa sababu anazozijua mwenyewe, atapigwa picha, alama za vidole na kumbukumbu zote muhimu zitachukuliwa na atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka.



Kova alisema mtu yeyote atakaeona kitendo cha uhalifu uwanjani hapo, atume ujumbe mfupi wa (sms) kwenye namba 0783034224, ambapo ujumbe huo utaingia katika kompyuta ya polisi itakayokuwepo uwanjani hapo na hatua zitachukuliwa mara moja.



Shirikisho la Soka nchini (TFF) kupitia kwa katibu mkuu wake Angetile Osiah lilisema jana kuwa halikuwa na taarifa juu ya tishio la Al-Shabaab kushambulia jijini Dar es Salaam kama ilivyoelezwa na Jeshi la Polisi lakini wanalifanyia kazi.



"Hatuna taarifa zozote, lakini kesho kutakuwa na kikao cha wadau wote wa mechi ya Jumamosi (kesho) hivyo tutajadili suala la hilo ili kuona tunachukua tahadhari zipi," alisema Osiah.



Alisema kuwa kikao hicho cha leo mbali na kuwahusisha viongozi wa Simba na Yanga, pia kitalishirikisha Jeshi la Polisi pamoja na maafisa wa Usalama wa Taifa.