MKUU wa Kituo cha Polisi Iyumbu na askari wa upelelezi katika kituo hicho, wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kupokea rushwa kutoka kwa mfugaji waliyembambikizia kesi.

Mkuu huyo, Koplo Lukololo na askari Konstebo Joseph Pazza, wanadaiwa kuchukua fedha za mfugaji huyo, Shigela Nkonga baada ya kumpekua na kumtuhumu kumkuta akimiliki silaha kinyume cha Sheria.

Mbali na umiliki wa silaha kinyume cha sheria, askari hao katika upekuzi huo uliofanyika
Oktoba 5, mwaka huu saa 4 asubuhi, walidai kumkuta mfugaji huyo na fuvu na mifupa ya binadamu na ngozi ya simba na chui.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Celina Kaluba alidai jana kuwa kutokana na tuhuma hizo, askari hao wanadaiwa kumtaka mfugaji huyo awape rushwa ya Sh milioni tisa ili wasimchukulie hatua za kisheria.

Kwa mujibu wa Kamanda Kaluba, maofisa wengine wa kijiji na kata wanadaiwa walitumika kumshinikiza mfugaji huyo kulipa fedha hizo ambao pia wanashikiliwa Polisi wakati upelelezi ukiendelea.

Kati ya maofisa hao, yupo Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nkongwa, Leonard Kahema, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Masuha, Sungwa Nkuba na mkazi wa Kijiji cha Iyumbu, Hussein Kayaka.

Baada ya kushinikizwa kutoa fedha hizo, kwa mujibu wa madai ya Kamanda Kaluba, mfugaji huyo alilazimika kuuza ng'ombe wake 31 na kuwapa askari hao kiasi hicho cha fedha walichokuwa wakikihitaji ili kumaliza mambo.



Kamanda Kaluba alisema kutokana na kuuzwa ng'ombe hao, wanakijiji wa Nkongwa hawakuridhika na wakaamua kulifikisha suala hilo Polisi ambako waliwakamata watuhumiwa.

Alisema baada ya upelelezi kukamilika, raia hao watatu watafikishwa mahakamani na askari hao wawili tayari wameshafikishwa kwenye mahakama ya kijeshi.

Alifafanua kuwa iwapo itagundulika askari hao walihusika, watafikishwa katika mahakama ya kiraia kuunganishwa na maofisa hao wa kitongoji na kijiji katika kesi itakayokuwa ikiwakabili.

Polisi hao wamekamatwa huku kukiwa na tuhuma za muda mrefu zinazolichafua Jeshi la Polisi kwa kuhusika katika kubambikizia kesi wananchi ili wapate rushwa.

Juzi katika Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi na Magereza nchini, iliwafukuzwa kazi kwa askari polisi kwa kosa la kuomba rushwa na kutaka kumbambikizia raia kesi na mwingine kwa kumjeruhi raia kwa kukusudia.

Wakati wa kuwafukuza polisi hao, Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha alinukuliwa akionya: “Tume hii itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria askari wote watakaobainika kukiuka maadili ya kazi zao.”

Alisema askari watakaoshughulikiwa bila huruma ni pamoja na wale watakaobainika kujihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa, kuwabambikizia kesi raia na kuvuruga utaratibu wa kuwatunza wafungwa magerezani.