Mwanafunzi wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Tosamaganga, mkoani Iringa, Frank Samson, ametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi, baada ya kukutwa akijiandaa kumfanyia mtihani wa Kiingereza mtahiniwa wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Mwembetogwa, Hussein Wanguvu.
Frank, alikamatwa muda mfupi jana asubuhi katika chumba cha mitihani cha shule ya Sekondari ya Mwembetogwa inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Manispaa ya Iringa.
Taarifa za kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo zilithibitishwa jana na Ofisa Elimu wa Mkoa wa Iringa, Joseph Mnyikambi, muda mfupi baada ya kutokea kwa tukio hilo.
“Huyu Frank ambaye anasoma masomo ya Sayansi (PCM) katika Sekondari ya Tosamaganga alikutwa na msimamizi mkuu wa kituo hicho akiwa kwenye chumba cha mitihani amevalia sare za Shule ya Mwembetogwa… na wakati huo tayari alikuwa ameshafanikiwa kuandikisha namba ya mtihani ya mtahiniwa wa kidato cha nne, Hussein Wanguvu aliyesajiliwa kwa namba S.0445/0147,” alisema Mnyikambi.
Ofisa elimu huyo alisema kwamba mtuhumiwa wa tukio hilo aligundulika kuwa siyo mtahiniwa halisi wa kituo hicho na kwamba alikusudia kumfanyia mtihani huo wa Kiingereza Hussein.
“Kwanza alidanganya jina lake na sehemu alikotokea mara baada ya mimi kufika katika eneo hilo muda na mfupi baadaye nilimhoji na akaniambia anasoma Tukuyu Sekondari huko Mbeya, lakini nikafanya maamuzi ya haraka na nilimpigia simu Ofisa Elimu wa mkoa huo, akaniambia hana mtu kama huyo, kwa hiyo ikabidi tumbane tena, ndipo akasema ukweli kuwa yeye anasoma PCM Sekondari ya Tosamaganga.
Hivi sasa tunavyoongea, nimesharipoti Baraza la Mitihani kuhusu tukio hilo,” alisema Mnyikambi.
Mtahiniwa ambaye alistahili kufanya mtihani huo alijitokeza eneo hilo muda mfupi na aliruhusiwa kufanya mtihani huo, baada ya kuhojiwa na Jeshi la Polisi.
Hata hivyo, Mnyikambi alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya msimamizi wa kituo hicho kubaini fomu yenye picha ya mtahiniwa, haiwiani na taswira ya aliyekuwa akitaka kufanya mtihani huo.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Evarist Mangalla, ili kupata taarifa za undani wa tukio hilo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kufafanua kuwa Polisi wanaendelea na uchunguzi.