Ndege ndogo aina ya Piper Pa 34-300 namba 5H-QTE, mali ya World Quality Travel and Tour Limited ikiwa imeanguka nyumbani kwa Maria Akyoo, Arumeru mkoani Arusha na kuua rubani na mbuzi watatu. (Picha na Prisca Libaga wa Maelezo).
RUBANI wa ndege ndogo aina ya Piper Pa 34- 300 namba 5H-QTE, mali ya World Quality
Travel and Tour Limited, Ally Harun (24), mkazi wa Arusha, amekufa huku rubani msaidizi
Lilian Koima, akijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC Kilimanjaro, baada ya ndege hiyo kuanguka Arumeru.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa, alisema ndege hiyo ilikuwa na marubani wawili ambao ni marehemu na mwenzake Lilian Koima, ambaye hajajulikana umri wake na makazi yake, wakitokea Dar es
Salaam na kuelekea uwanja wa ndege wa Arusha.
Alisema ndege hiyo ikiwa angani saa 1.46 usiku na ikiwa imekaribia uwanja wa Arusha kutua, ilishindwa kutua kwa sababu ya giza nene kutanda uwanjani hapo na kulazimika kubaki angani.
“Wakati wakiwa angani mmoja wa rubani hawa akapiga simu Tower Control wa Uwanja wa (KIA) na kuomba kutua huko, nao aliwaruhusu na wakiwa njiani kuelekea huko, ilianguka katika kijiji cha Samaria kata ya Kikatiti, Arumeru na mawasiliano yakakatika ghafla kati yao na KIA,” alisema Mpwapwa.
Alisema ndege hiyo ilianguka karibu na nyumba ya Maria Akyoo na kuharibika na kuua mbuzi watatu walioangukiwa papo hapo, pia kibanda cha biashara kiliharibiwa.
Kamanda Mpwapwa alisema Ally alikufa papo hapo huku Lilian akijeruhiwa na kukimbizwa KCMC. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.
Alisema chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana na Polisi inaendelea na uchunguzi. Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Arusha, Simon Kimiti, alisema kwa njia ya simu kuwa hatakiwi kujibu lolote na anayetakiwa kuzungumzia suala hilo ni watu wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa
Kilimanjaro - KIA.
Taarifa ya Wizara ya Uchukuzi iliyotolewa jana ilisema ndege hiyo yenye injini mbili na uwezo wa kubeba abiria sita ni mali ya Mawala Advocates na ilikuwa ikisafiri kutoka Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam kwenda Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa Edward Mkiaru aliyesaini barua hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya
Uchukuzi, wakaguzi wa ajali za ndege kutoka Wizara hiyo wako Kilimanjaro kuchunguza chanzo cha ajali.
0 Comments