BAADHI ya wafanyabiashara katika maeneo ya Himo, Holili na Tarakea katika Wilaya ya za Moshi na Rombo, wamebuni mbinu mpya ya usafirishaji wa sukari kwenda nchini Kenya
ambapo sasa sukari huwekwa katika dumu za mafuta ya kula na ndoo za maji ya kunywa.

Katika mbinu hiyo wafanyabiashara humimina sukari kwenye dumu hizo za lita 20 na kisha kumwaga mafuta kidogo juu ya dumu hizo ili kuashiria kilichobebwa ni mafuta huku pia wakisafirisha sukari katika ndoo za maji ili kukwepa mitego ya polisi.

Mmoja wa wakazi wa Tarakea aliyejitambulisha kwa jina moja la Massawe alisema baadhi ya wasafirishaji wa sukari hiyo kwa njia za panya, pia hubeba mifuko mitupu ya sukari ambayo baadaye hutumika tena kuhifadhi sukari hiyo mara iingiaapo nchini Kenya.

“Zipo baadhi ya nyumba hapa Tarakea zimegeuzwa maghala ya sukari, inasafirishwa kwa ndoo na dumu za mafuta na ikifika Kenya hushonwa upya katika ujazo wa kilo 25 na 50, huwezi kugundua kwani hushonwa kitaalamu na hurejea kama awali inapotoka kiwandani,” alisema.

Alisema vyombo vya usafiri vinavyotumika kusafirishia ni baiskeli, pikipiki na gari ambapo mfuko wa kilo 50 huuzwa kwa wastani wa Sh 130,000 hadi Sh 250,000 jambo linalowavutia vijana wengi kufanya biashara hiyo.

Baadhi ya wananchi waliozungumza walidai kununua bidhaa hiyo kwa wastani wa Sh 2,700 hadi Sh 3,500 kwa kilo ingawa pia wakati mwingine huwa haipatikani madukani.

Hivi karibuni serikali iliwafutia leseni za usambazaji sukari makampuni matatu mkoani Kilimanjaro kwa madai yanachangia kuadimika kwa bidhaa hiyo sokoni na uuzwaji nje nchi kinyume na maelekezo ya serikali.

Kufuatia hali hiyo serikali ilikabidhi jukumu hili kwa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa kahawa mkoani Kilimanjaro( KNCU) na kampuni nyingine ya Modern ili kusambaza bidhaa hiyo na kuhakikisha bei inashuka kutoka bei ya sasa hadi bei elekezi ya Serikali ya Sh 1,900.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni Mwenyekiti wa KNCU, Maynard Swai alisema chama chake kimesambaza sukari hiyo kupitia vyama 22 kati ya 92 ingawa bado kuna changamoto katika kudhibiti suala la bei.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama alipohojiwa kwa njia ya simu kuhusiana na kuadimika kwa bidhaa hiyo sokoni alikiri hali hiyo na kueleza kuwa jana alitarajia kukutana na wasambazaji na Kiwanda cha TPC ili kujadili suala hilo.