Wachezaji wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, wakiingia kwenye basi muda mfupi baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam wakitokea nchini Morocco katika mchezo wa kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika. Stars walifungwa na Morocco mabao 3-1. (Picha na Fadhili Akida).
KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen amesema hapati shinikizo lolote kutokana na kauli ya
aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mbrazili Marcio Maximo kwamba yuko tayari kurudi kufundisha Stars.
Maximo alinukuliwa na gazeti hili akisema yupo tayari kurudi nchini kuifundisha Taifa Stars, kama Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakimhitaji kufanya hivyo.
Akizungumza Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam jana baada ya Stars kurejea ikitokea Morocco ilikofungwa mabao 3-1 Jumapili na kushindwa kufuzu fainali za Afrika mwakani, alisema hasumbuliwi na kauli hiyo kwani bado ana mkataba wa miaka miwili wa kuifundisha Stars.
“Sina presha na alichokisema kocha huyo, zaidi ya yote bado nina mkataba wa miaka miwili wa kuifundisha timu hii na ninachoangalia ni kuiandaa timu kwa ajili ya michuano ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia,” alisema Poulsen.
Maximo alikaririwa juzi pamoja na mambo mengine akikosoa utaratibu wa sasa wa kutoinua vijana na badala yake kuita katika timu ya Taifa wachezaji wakongwe kwa sababu tu wanaishi Ughaibuni.
Pia alishangaa kusikia kuwa hivi sasa Mrisho Ngassa anakalishwa benchi katika timu ya Taifa na kuingia baadaye, wakati ni mchezaji mahiri na kusema kuwa kufanya hivyo ni kuua kiwango chake.
Tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema linasubiri ripoti ya kocha huyo ili kujua nini kifanyike kuboresha timu hiyo.
Hata hivyo akizungumza jana kuhusu Stars kushindwa kufuzu fainali hizo, Poulsen alisema, wamefungwa na timu bora yenye wachezaji wengi wanaocheza Ulaya na Ligi Kuu ya England.
Poulsen alisifu kiwango kilichooneshwa na timu yake kwa kudai kuwa wachezaji wake walionesha mchezo mzuri na kujituma muda wote.
Akizungumzia mchezo ujao dhidi ya Chad kuwania kuingia makundi ya mchujo kwa ajili ya michezo ya kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2014, Poulsen alisema atabadilisha kidogo kikosi hicho na kwamba wachache kati ya wachezaji waliopo sasa ndio watakaokosekana.
“Nitawezaje kubadili kikosi chote? Haiwezakani, wengi watakuwepo wachache watakosekana,” alisema Poulsen.
0 Comments