Alipekuliwa maungoni, akavuliwa viatu, koti
Wapekuzi hawakujali ni mwanadiplomasiaRais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, amesema Tanzania inanuka nje ya nchi kutokana na tuhuma za usafirishaji wa dawa za kulevya na kwamba kuporomoka kwa sifa ya nchi kulipata kumuathiri akiwa ughaibuni.

Mwinyi aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa Baraza la Viongozi wa Dini la Kupambana na Athari za Dawa za Kulevya.
Alisema aliathirika na tuhuma za dawa za kulevya wakati akisafiri kwenda Ujerumani akiwa ameongozana na msafara wa watu 10 wakati akibadili ndege katika nchi ambayo hakuitaja.
Alisema maofisa uhamiaji wa nchi hiyo walimfanyia upekuzi kama inavyotakiwa, lakini mmoja wa maofisa hao aliamua kumfanyia upya upekuzi katika chumba kingine tofauti.
Akisimulia mkasa huo, alisema kuwa alipoingizwa kwenye chumba hicho, ofisa huyo alimuamuru kuvua viatu na kumpekua na kama hiyo haikutosha, alimuamuru avue koti na kuzidi kumpekua zaidi.
Mwinyi aliwaeleza waliohudhuria uzinduzi huo kuwa mmoja kati ya wasaidizi wake aliofuatana nao katika ziara hiyo, alimwambia ofisa huyo kuwa yeye (Mwinyi), ana hadhi ya kidiplomasia, lakini ofisa huyo alijibu kwa jeuri kwamba hilo hajali.
Mzee Mwinyi aliendelea kusimulia kuwa baada ya kukaguliwa sana, waliruhusiwa kuondoka na aliamua kumzawadia ofisa huyo tasbihi aliyokuwa ameishika mkononi.
Alieleza kuwa baadaye alipojiuliza na kugundua kuwa sababu iliyosababisha apekuliwe sana ni kushika tasbihi.
Aliongeza kuwa viongozi wa dini ni miongoni mwa watu wanaotuhumiwa sana kusafirisha dawa za kulevya wakiwemo wa kutoka Tanzania.
“Nilishangaa sana upekuzi ule na ndipo nilipojiuliza maswali na baadaye kugundua kuwa tasbihi ile ndiyo iliyoniponza kwa kuwa maneno mengi yanasemwa na hasa wacha Mungu Watanzania wanadaiwa kuwa ndio wafichaji na wasafirishaji wa dawa za kulevya,” alisema na kuongeza kuwa:
“Lakini nilimsamehe ofisa yule ila nilijifunza kuwa Watanzania tunanuka nje ya nchi na kadiri unavyovaa majoho mengi ndivyo wanavyozidi kukutilia shaka zaidi.”
Mwinyi aliishukuru Taasisi ya Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa ya Wizara ya Afya na Marekani kwa mchango na msaada wao katika kuwasaidia vijana wa Tanzania kuepukana na matumizi ya dawa za kulevya.
KAULI YA WAZIRI LUKUVI
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema Baraza hilo limezinduliwa katika wakati mwafaka kwani viongozi wa dini wana ushawishi mkubwa kwa jamii katika vita dhidi ya dawa za kulevya.
Alisema hiyo inatokana na viongozi wa dini hutumia maandiko na mahubiri yao tofauti na serikali inayotumia mabavu na shuruti.
Lukuvi aliongeza kuwa serikali iko tayari kushirikiana na Tume ya Kupambana na Dawa za Kulevya pamoja na Baraza hilo ili kukamata zaidi watuhumiwa wa dawa za kulevya.
Waziri huyo alisema biashara ya dawa za kulevya ina ushawishi mkubwa katika jamii kwa kuwa wapo watu mbalimbali walioshika nafasi za uongozi duniani kwa kusaidiwa na dawa hizo, akiwemo aliyekuwa Rais wa Panama, Manuel Noriega.
Aidha, Lukuvi alishauri sheria za kudhibiti dawa za kulevya zibadilishwe ili iwe moja na kutaka kila atakayekamatwa nazo kufungwa kifungo cha maisha na kufilisiwa mali.
“Sheria zilizopo hazifai kwani wanaofanya biashara hizi wana hela kwa hiyo ni rahisi kwa mtuhumiwa kulipa faini yoyote ile atakayotajiwa na mahakama tofauti na kifungo ambacho wengi wataogopa kufungwa maisha,” alisema Lukuvi.

KAMISHNA: BIASHARA HII HATARI
Naye Kamishna wa Tume ya Dawa za Kulevya, Christopher Shekiondo, alisema biashara ya dawa za kulevya ni hatari kwa ustawi wa taifa lolote kwani dunia inashuhudia mauaji, vurugu na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe katika baadhi ya nchi kama ilivyo sasa nchini Mexico ambapo wafanyabiashara wa dawa hizo wanapigana na vyombo vya dola vya nchi hiyo.
Shekiondo alisema biashara hiyo huzalisha fedha nyingi haramu na kuwafanya wahalifu wa biashara hiyo kujipenyeza katika uongozi wa kisiasa katika ngazi mbalimbali kwa lengo la kulinda maslahi ya biashara zao, jambo ambalo ni hatari sana kwa ustawi wa jamii husika.
Kamishna Shekiondo alisema takwimu zinaonyesha kuwa huko nyuma walikamata idadi ndogo ya dawa za kulevya, lakini hivi karibuni idadi imeongezeka kwa sababu serikali imejizatiti na wananchi wanatoa msaada mkubwa kwa kutoa taarifa kwa njia ya simu, mtandao na ujumbe mfupi wa simu za mkononi.
Alisema katika kipindi kifupi cha kuanzia mwaka 2008 mpaka 2011, watuhumiwa 22,814 walikamatwa nchini na wengine 67 walikamatwa nje ya nchi kwa kujihusisha na biashara hiyo.
Aliongeza kuwa kuanzia mwaka 2000 hadi 2009, kilo 57 za cocaine zilikamatwa zikilinganishwa na kilo 191 za cocaine zilizokamatwa katika kipindi kifupi cha Januari, 2010 hadi Septemba, 2011, huku kilo 164 za heroin zilikamatwa zikilinganishwa na kilo 453 za dawa hizo zilizokamatwa kati ya Januari, 2010 na Septemba, 2011.
Naye Mwenyekiti wa Baraza hilo, Sheikh Mussa Salum, aliishukuru Tume kwa kutambua mchango wa viongozi wa dini kwa kuwa taifa litaendelea kupoteza nguvu kazi kama hatua hazitachukuliwa.
Alisema viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika jamii na kwamba dini zote zikishirikiana na kutoa elimu ya kutosha tatizo hilo linaweza kutoweka. Alisema vitabu vyote vitakatifu vinakataza matumizi ya dawa za kulevya.