IKULU imekanusha taarifa kwamba Rais Jakaya Kikwete ametoa msamaha wa adhabu ya kifo iliyowakabili askari Polisi wa zamani waliopatikana na hatia ya kumuua aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Luteni Jenerali Imran Kombe, mwaka 1996.

“Masuala yote yanayohusu polisi hao waliohukumiwa kifo kwa mauaji ya Luteni Jenerali Kombe yalifanyiwa maamuzi kabla ya Rais Kikwete kuingia madarakani Desemba 21, 2005,” ilisema taarifa ya Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais, Ikulu jana kwa vyombo vya habari.

Ikulu ilikuwa ikizungumza taarifa za gazeti la Mwananchi, matoleo ya juzi na jana, zilizodai kuwa Rais Kikwete alitoa msamaha wa kupunguza adhabu ya kifo iliyowakabili askari Polisi hao
waliopatikana na hatia ya kumpiga risasi na kumwua kwa makusudi Luteni Jenerali Imran Kombe Juni 30, 1996.

“Gazeti hili (Mwananchi) limedai kuwa Mheshimiwa Rais Kikwete alitoa msamaha huo kwa kupunguza adhabu ya kifo iliyokuwa inawakabili makonstebo wapelelezi Mataba Matiku na
Juma Muswa na kuibadilisha kuwa kifungocha miaka miwili.

“Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, inapenda kufafanua kuwa Mheshimiwa Rais Kikwete hajawahi na hajapata kuhusika hata kidogo kutoa msamaha wa kirais kwa kupunguza adhabu
ya wauaji hao wa Luteni Jenerali Kombe tokea kuingia madarakani,”ilisema taarifa hiyo.